< Kutoka 32 >

1 Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Aruni, wakamwambia, “Njoo, katufanyizie sanamu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.” 2 Hivyo Aruni akawaambia, “Zitoeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.” 3 Watu wote wakavua pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, na wakamletea Aruni. 4 Akapoke mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha. Nao wakasema, “Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.” 5 Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Aruni akatangaza akasema, 6 “Kesho itakuwa sikukuu kwa Yahweh.” Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze. 7 Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Shuka upesi, kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao. 8 Wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu. Wakasema, 'Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. 9 Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu. 10 Basi sasa usinizuie. Ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize. Nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.” 11 Musa akamsihi sana Yahweh Mungu wake, na kusema,”Yahweh, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri kusema, 'Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi?' Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. 13 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, 'Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.'” 14 Na Yahweh akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake. 15 Kisha Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake. Mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. 16 Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. 17 Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna kelele ya vita kambini. 18 “Lakini Musa akasema, “Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.” 19 Hata alipoyakaribia kambini akaiona ile ndama, na watu wakicheza. Hasira ya Musa ikawaka. Akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. 20 Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji. Akawanywesha wana wa Israeli. 21 Musa akamwambia Aruni, “Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? 22 Aruni akasema, “Hasira yako isiwake, bwana wangu. Wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. 23 Maana waliniambia, 'Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu. Kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.' 24 Nikawaambia, 'Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivue; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.” 25 Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi (maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao) 26 Ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, “Mtu awaye yote aliye upande wa Yahweh na aje kwangu.” Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia. 27 Akawaambia, Yahweh, Mungu wa Israeli, asema hivi, 'Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake.'” 28 Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu. 29 Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa Yahweh leo, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili Yahweh awape baraka leo.” 30 Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kuu. Sasa nitakwenda juu kwa Yahweh. Labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.” 31 Musa akarejea kwa Yahweh akasema,” Oh! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. 32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.” 33 Yahweh akamwambia Musa, “Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. 34 Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Lakini pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.” 35 Kisha Yahweh akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Aruni aliifanya.

< Kutoka 32 >