< Kutoka 3 >

1 Wakati huu Musa aliendelea kuchunga mifugo ya Yethro baba mkwe wake, kuhani wa Midiani. Musa aliliongoza kundi la mifugo kuelekea upande wa mbali wa jangwa mpaka kufika Horebu, mlima wa Mungu. 2 Akiwa pale malaika wa Yahwe akamtokea kama mwali wa moto katika kichaka. Musa aliangalia, na tazama, kichaka kiliwaka moto lakini hakikuteketea. 3 Musa akasema, “Nitageuka ili nione kitaku hiki cha ajabu, kwa nini kichaka hakiteketei.” 4 Yahwe alipoona ya kuwa amegeuka upande ili aone, Mungu alimwita kutoka katika kile kichaka na kusema, “Musa, Musa.” Musa akasema, “Mimi hapa.” 5 Mungu akasema, “Usinikaribie! Vua viatu katika miguu yako, kwa kuwa mahali uliposimama ni mahali palipowekwa wakfu kwa ajili yangu.” 6 Aliongeza kusema, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Kisha Musa akaufunika uso wake, kwa kuwa aliogopa kumwangalia Mungu. 7 Yahwe akasema, “Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri. Nimesikia kelele zao kwa sababu ya mabwana wao, kwa kuwa nayajua mateso yao. 8 Nimekuja chini kuwaokoa dhidi ya mamlaka ya Wamisri na kuwatoa katika nchi ile na kuwaleta katika nchi nzuri, pana, nchi ijaayo maziwa na asali; kwenye ukanda wa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi. 9 Sasa kilio cha watu wa Israeli kimenifikia mimi. Zaidi sana, Mimi nimeyaona mateso ambayo Wamisri wanawatesa. 10 Sasa basi, nitakutuma wewe kwa Farao ili upate kuwatoa watu wangu, wana wa Israeli, kutoka katika nchi ya Misri.” 11 Lakini Musa akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao na kuwatoa Waisraeli kutoka Misri?” 12 Mungu akamjibu, “Hakika nitakuwa pamoja nawe. Hii itakuwa ishara kwako ya kuwa nimekutuma. Utakapokuwa umewatoa watu kutoka Misri, mtaniabubu mimi katika mlima huu.” 13 Musa akamwambia Mungu, “Nikienda kwa Waisraeli na kuwaambia, 'Mungu wa baba zenu amenituma mimi kwenu,' na kisha wakiniambia, 'jina lake nani?' nitawaambia nini?” 14 Mungu akamwambia Musa, “MIMI NIPO AMBAYE NIPO.” Mungu akasema, “Ni lazima uwaambie Waisraeli, “MIMI NIPO amenituma kwenu.” 15 Pia Mungu akamwambia Musa, “Lazima uwaambie Waisraeli, 'Yahwe, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo amenituma mimi kwenu. Hili ndio jina langu milele, na hivi ndivyo nitakavyokumbukwa na vizazi vyote.' 16 Nenda ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja. Waambie, 'Yahwe, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, wa Isaka na Yakobo, amenitokea mimi na kusema, “Hakika nimewatazama na nimeona yale mliyotendewa huko Misri. 17 Nimeahidi kuwatoa ninyi katika mateso ya Misri na kuwaleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Wamwori, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi. Nchi ijaayo maziwa na asali.” 18 Watakusikiliza. Wewe pamoja na wazee wa Israeeli itawapasa kwenda kwa mfalme wa Misri, na imewapasa kumwambia, 'Yahwe, Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Hivyo tuache sisi twende safari ya siku tatu katika jangwa ili tupate kutoa sadaka kwa Yahwe Mungu wetu.' 19 Lakini nafahamu ya kuwa mfalme wa Misri hatawaacha ninyi mwende, isipokuwa kwa kulazimishwa. 20 Nitainua mkono wangu na kuwapiga Wamisri kwa miujiza yote nitakayoifanya kati yao. Baada ya hayo, atawaacha mwende. 21 Nitawapa watu hawa kufadhiliwa kutoka kwa Wamisri ili muondokapo msiende mikono mitupu. 22 Kila mwanamke ataomba kwa jirani yake Mmisri na kwa kila mwanamke akaaye kwenye nyumba ya jirani yake, vyombo vya fedha na vya dhahabu na nguo. Nanyi mtawavika watoto wenu wa kiume na binti zenu. Kwa njia hii mtawateka nyara Wamisri.”

< Kutoka 3 >