< Kutoka 27 >

1 Nawe fanya madhabahu ya mti wa mshita, urefu wake utakuwa ni dhiraa tano na upana wake dhiraa tano. Hiyo madhabahu itakuwa mraba na kwenda juu kwake kutakuwa dhiraa tatu. 2 Nawe fanya pembe nne kama mfano wa pembe za ng'ombe. Hizo pembe zitakuwa za kitu kimoja na madhabahu, nawe utayafunika kwa shaba. 3 Lazima vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake. Vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba. 4 Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba. Kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu. 5 Nawe lazima uweke huo wavu chini ya kizingo kiizungukacho madhabahu upande wa chini. 6 Nawe fanya miti kwa ajili ya madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba. 7 Na hiyo miti itatiwa katika viduara, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukua. 8 Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake kama ulivyooneshwa mlimani. 9 Nawe ufanye ua wa maskani. Upande wa kusini wa kuelekea kusini kutakuwa na chandarua ya nguo ya kitani nzuri yenye kusokotwa, kwa huo ua, urefu wake upande mmoja utakuwa ni dhiraa mia moja. 10 Na nguzo zake zitakuwa nguzo ishirini, na vitako vyake ishirini, vitako vyake vitakuwa vya shaba kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 11 Ni vivyo hivyo upande wa kaskazini, urefu wake hiyo chandarua utakuwa ni dhiraa mia moja, na nguzo zake ishirini, na vitako vyake ishirini vitakuwa vya shaba, kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 12 Na upande wa magharibi, upana wa ua kutakuwa na chandarua ya dhiraa hamsini; nguzo zake kumi, na vitako vyake kumi. 13 Na upana wa ule ua upande wa mashariki kuelekea mashariki utakuwa ni dhiraa hamsini. 14 Chandarua upande mmoja wa lango itakuwa dhiraa kumi na tano upana wake. Lazima nguzo zake zitakuwa tatu na vitako vyake vitatu. 15 Upande wa pili ni vivyo hivyo chandarua ya dhiraa kumi na tano; nguzo zake tatu, na vitako vyake vitatu. 16 Na kwa lile lango la ua patakuwa na kisitiri cha dhiraa ishirini, kitakuwa cha nguo ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshonaji taraza; nguzo zake zitakuwa nne, na vitako vyake vinne. 17 Nguzo zote za ule ua ziuzungukao pande zote zitakuwa na vitanzi vya fedha; kulabu zake za fedha, na vitako vyake vya shaba. 18 Urefu wa huo ua utakuwa dhiraa mia moja, na upana wake utakuwa dhiraa hamsini kotekote, na kwenda juu kwake dhiraa tano; yawe ya nguo ya kitani nzuri, na vitako vyake vitakuwa vya shaba. 19 Vyombo vyote vya maskani vitumiwavyo katika utumishi wake wote, na vigingi vyake vyote, na vigingi vyote vya ule ua, vitakuwa vya shaba. 20 awe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima. 21 Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hadi asubuhi mbele ya BWANA; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.

< Kutoka 27 >