< Torati 29 >

1 Haya ni maneno ambayo Yahwe alimuamuru Musa kuwaambia watu wa Israeli katika nchi ya Moabu, maneno ambayo yaliongezwa katika agano alilolifanya pamoja nao kule Horebu. 2 Musa aliwaita Waisraeli wote na kuwaambia, “Mmeona kila kitu ambacho Yahwe alifanya mbele ya macho yenu katika nchi ya Misri kwa Farao, kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote – 3 mateso makubwa ambayo macho yenu yaliona, ishara, pamoja na ile miujiza mikubwa. 4 Lakini mpaka leo Yahwe hajawapatia moyo wa kufahamu, macho ya kuona, au masikio ya kusikia. 5 Nimewaongoza kwa miaka arobaini jangwani; mavazi yenu hayakuchakaa juu yenu, na ndala zenu hazikuchakaa miguuni mwenu. 6 Hamkula mkate wowote, na wala hamkunywa divai yoyote au kinywaji chochote chenye ulevi, ili kwamba muweze kujua kuwa mimi ni Yahwe Mungu wenu. 7 Mlipokuja mahali hapa, Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, walikuja dhidi yetu kutupiga, na tukawapiga. 8 Tulichukua ardhi yao na kuwapa kama urithi Wareubeni, kwa Wagadi, na kwa nusu ya kabila ya Manase. 9 Kwa hiyo shikilia maneno ya agano hili na kuyatenda, ili ufanikiwe katika kila kitu ufanyacho. 10 Nyie wote, mnasimama leo, mbele ya Yahwe Mungu wenu; machifu wenu, makabila yenu, wazee wenu, na maafisa wenu – wanaume wote wa Israeli, 11 watoto wenu, wake zenu, na wageni ambao wamo miongoni wa kambi yenu, kutoka kwa yule anayekata mbao zenu mpaka kwa yule atekaye maji. 12 Mpo hapa ili kwamba muingie katika agano la Yahwe Mungu wenu na katika kiapo ambacho Yahwe Mungu wako anafanya na wewe leo, 13 ili kwamba awafanye leo kuwa watu wake, na kwamba aweze kuwa Mungu kwa ajili yako, kama alivyonena kwako, na kama alivyoapa kwa mababu zako, kwa Abrahamu, kwa Isaka na kwa Yakobo. 14 Kwa maana ninafanya agano hili na kiapo hiki sio na wewe tu – 15 pamoja kila mtu aliyesimama hapa pamoja nasi leo mbele ya Yahwe Mungu wetu – bali na wale ambao hawapo pamoja nasi leo pia. 16 Unajua jinsi tulivyoishi katika nchi ya Misri, na jinsi tulivyopenya miongoni mwa mataifa ambao uliwapita. 17 Mmeona sanamu zao zinazokera zilizotengenezwa kwa mbao na mawe, fedha na dhahabu, ambazo zilikuwa miongoni mwenu. 18 Hakikisha hakuna kati yenu mwanamume, mwanamke, ukoo, au kabila ambaye moyo wake unamuacha Yahwe Mungu wetu leo, ili kwenda na kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisha hakuna kati yenu mzizi utakaozaa nyongo na pakanga. 19 Wakati mtu huyo anaposikia maneno ya laana hii, atajifariji moyoni mwake na kusema, “Nitakuwa na amani, ingawa natembea katika ukaidi wa moyo wangu”. Hii itaangamiza ubichi pamoja na ukavu. 20 Yahwe hatamsamehe, lakini badala yake, hasira ya Yahwe na wivu wake utambanika mtu huyo, na laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki vitakuwa juu yake, na Yahwe ataliondoa jina lake kutoka mbinguni. 21 Yahwe atamuweka kando kwa ajili ya maafa kutoka katika makabila yote ya Israeli, kwa kuzingatia laana zote za agano ambazo zimeandikwa katika kitabu hiki cha sheria. 22 Kizazi kifuatacho, watoto wako watakaoinuka baada yako, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watazungumza watakapoona mapigo juu ya nchi hii na magonjwa ambayo Yahwe ameyafanya yawe – 23 na watakapoona kuwa nchi yote imekuwa salfa na chumvi ichomayo, ambapo hakuna kitu kipandwacho au kuzaa matunda, ambapo hapaoti mmea wowote, kama anguko la Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambayo Yahwe aliangamiza katika ghadhabu na hasira yake – 24 watasema kwa pamoja na mataifa mengine, “Kwa nini Yahwe amefanya hili katika nchi hii? Joto ya hasira hii kali inamaanisha nini?” 25 Kisha watu watasema, “Ni kwa sababu walitelekeza agano la Yahwe, Mungu wa mababu zao, alilofanya nao alipowatoa kutoka Misri, 26 na kwa sababu waliondoka na kutumikia miungu mingine na kuzisujudu, miungu ambayo hawakujiua na ambayo hakuwapatia. 27 Kwa hiyo hasira ya Yahwe imewaka dhidi ya nchi hii, ili kuleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. 28 Yahwe amewang’oa kutoka nchini kwao kwa hasira, kwa ghadhanu, na kwa ghadhabu kali, na kuwatupa katika nchi nyingine, leo. 29 Mambo ya siri ni ya Yahwe Mungu wetu pekee; lakini mambo yaliyofichuliwa ni ya kwetu milele pamoja na wazawa wetu, ili tufanye maneno yote ya sheria hii.

< Torati 29 >