< Torati 21 >

1 Iwapo mtu amekutwa kauwawa ndani ya nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kumiliki, kalala shambani, na haijulikani aliyemshambulia; 2 basi wazee wenu pamoja na waamuzi wenu wanapaswa kutoka nje, na kupima katika miji ambayo inamzunguka yule aliyeuawa. 3 Kisha wazee wa mji ulio karibu na mwili wa marehemu wanapaswa kuchukua mtamba kutoka kwenye kundi la mifugo, ambaye hajawahi kutumikishwa, wala kubebeshwa nira. 4 Kisha wanapaswa kumuongoza mtamba huyo mpaka chini ya bonde litiririkalo maji, bonde ambalo halijawahi kulimwa wala kupandwa, na mle bondeni wanapaswa kuvunja shingo ya mtamba huyo. 5 Makuhani, uzao wa Lawi, wanapaswa kuja mbele, kwa maana Yahwe Mungu wako amewachagua wamtumikie yeye na kutoa baraka katika jina la Yahwe na kuamua kila mtafaruku na ugomvi kwa neno lao. 6 Wazee wote wa mji ulio karibu na mtu aliyeuawa wanapaswa kunawa mikono yao juu ya mtamba aliyevunjwa shingo bondeni; 7 na wanapaswa kutoa suhulisho juu ya jambo hilo na kusema, ‘Mikono yetu haijamwaga damu hii, wala macho yetu hayajaona suala hili. 8 Tusamehe watu wako Israeli, Yahwe, ambao umewakomboa, na usiweke hatia juu ya umwagaji damu usio na kosa miongoni mwa watu wako Israeli.’ Kisha umwagaji damu utasamehewa kwao. 9 Kwa njia hii utaweka mbali umwagaji damu usio na hatia miongoni mwenu, mtakapofanya yaliyo mema machoni pa YAHWE. 10 Utakapokwenda kupigana vita dhidi ya maadui zako na Yahwe Mungu wako atakapokupa ushindi na kuwaweka chini ya mamlaka yako, na ukawachukua mbali kuwa mateka, 11 kama kati ya mateka ukamwona mwanamke mzuri, nawe ukamtamani na kutaka kujitwalia awe mke wako, 12 basi utamleta nyumbani kwako; atanyoa nywele zake na kukata kucha zake. 13 Kisha atazivua nguo alizokuwa amezivaa wakati alipochukuliwa mateka na atabaki nyumbani kwako na kuwaomboleza baba yake na mama yake kwa mwezi mzima. Baada ya hapo unaweza kulala naye na kuwa mume wake, naye atakuwa mke wako. 14 Lakini usipofurahishwa naye, basi unatakiwa kumruhusu aondoke apendaye yeye. Lakini haupaswi kamwe kumuuza kwa fedha, pia haupaswi kumfanya kama mtumwa, kwa sababu umemdhalilisha. 15 Iwapo mwanamume ana wake wawili na mmoja wao ampenda na mwingine kumchukia, na wote wamekwisha mzalia watoto –wote mwanamke mpendwa na mwanamke achukiwae – 16 basi katika siku ambayo mwanamume atakapowarithisha mali zake wanawe, hapaswi kumfanya mwana wa mke ampendaye kuwa mzawa wa kwanza kabla ya mwana wa mke amchukiaye, ambaye ndiye mwana wa kwanza. 17 Badala yake, anapaswa kumtambua mwana wa kwanza, mwana wa mke asiyempenda, kwa kumpatia mara mbili ya mali zake; kwa maana huyo mwana ni mwanzo wa nguvu zake; haki za mzawa wa kwanza ni zake. 18 Iwapo mwanamume ana mwana mkaidi na muasi ambaye hatatii sauti ya baba yake au sauti ya mama yake, ambaye, hata baada ya kurekebishwa, hatawasikia; 19 basi baba yake na mama yake wanapaswa kumshika na kumleta mbele ya wazee wa mji na kwenye malango ya mji. 20 Wanapaswa kuwaambia wazee wa mji, “Huyu mwanetu ni mkaidi na muasi; hataki kusikia sauti zetu; ni mwasherati na pia ni mlevi’. 21 Kisha wanaume wote wa mji wanapaswa kumpiga kwa mawe hadi kufa; nanyi mtaondoa uovu miongoni mwenu. Israeli yote itasikia juu ya hili na kuogopa. 22 Iwapo mwanamume kafanya dhambi inayostahili kifo na kisha akauwawa, kwa kunyongwa juu ya mti, 23 basi mwili wake haupaswi kubaki usiku kucha juu ya mti. Badala yake, unapaswa kuhakikisha unamzika siku hiyo; kwa maana yeyote anyongwaye amekwisha laaniwa na Mungu. Tii amri hii ili kwamba usitie najisi nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kama urithi.

< Torati 21 >