< Danieli 1 >

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja Yerusalemu na kuuzunguka mji ili kuzuia mahitaji yake yote.
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi.
2 Bwana alimpa Nebukadneza ushindi dhidi ya Yehoyakimu mfalme wa Yuda, na alimpatia vitu vitakatifu kutoka nyumba ya Mungu. Alivipeleka vitu hivyo mpaka katika nchi ya Babeli, kwa nyumba ya mungu wake, na aliviweka vitu vitakatifu katika hazina ya mungu wake.
Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
3 Mfalme akamwambia Ashipenazi, afisa wake mkuu, awalete baadhi ya watu wa Israeli, wa familia ya kifalme na za kiungwana -
Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu,
4 vijana wasio na hila, wenye mwonekano wa kuvutia, wenye ujuzi katika hekima yote, wenye kujawa na ufahamu na weledi, na wenye sifa za kutumika katika ikulu ya mfalme. Alitakiwa kuwafundisha maandiko na lugha ya Babeli.
vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo.
5 Mfalme aliwatengea kwa ajili yao fungu kutoka katika chakula chake kizuri kwa kila siku na katika divai aliyokunywa. Vijana hawa walitakiwa kufunzwa kwa miaka mitatu, na baada ya hapo, wangeweza kumtumikia mfalme.
Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
6 Miongoni mwao walikuwa ni Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria, baadhi ya watu wa Yuda.
Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria.
7 Afisa mkuu aliwapa majina: Danieli alimwita Belteshaza, Hanania alimwita Shadraka, Mishaeli alimwita Meshaki, na Azaria alimwita Abedinego.
Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.
8 Lakini Danieli alinuia katika akili yake kuwa asingejitia ujanisi mwenyewe kwa chakula kizuri cha mfalme wala kwa divai ambayo alikunywa.
Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii.
9 Basi, aliomba ruhusa kutoka kwa afisa mkuu ili kwamba asije akajitia uchafu yeye mwenyewe. Hivyo, Mungu alimpa Danieli kibali na huruma kupitia katika heshima ambayo afisa mkuu alikuwa nayo kwake.
Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli,
10 Afisa mkuu alimwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme. Ameagiza aina ya chakula na vinywaji mnavyotakiwa kutumia. Kwa nini awaone ninyi mkiwa mnaonekana vibaya kuliko vijana wengine wa umri wenu? Mfalme aweza kukitwaa kichwa changu kwa sababu yenu.
lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”
11 Kisha Daniel akamwambia msimamizi ambaye afisa mkuu alikuwa amemweka juu ya Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria.
Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria,
12 Alisema, “Tafadhari tujaribuni, sisi watumishi wako kwa siku kumi. Tupatieni tu mboga mboga za kula na maji ya kunywa.
“Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa.
13 Kisha ulinganishe mwonekano wetu na mwonekano wa vijana wanaokula vyakula vya mfalme, na mtutendee, sisi watu wako kulingana na kile unachokiona.”'
Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.”
14 Hivyo msimamizi alikubaliana naye kufanya hivi, na aliwajaribu kwa siku kumi.
Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.
15 Katika mwisho wa siku kumi mwonekano wao ulikuwa ni wenye afya nzuri kuliko wa wale vijana waliokula vyakula vya kifalme.
Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko yeyote kati ya wale vijana waliokula chakula cha mfalme.
16 Basi, msimamizi aliliondoa fungu lao la chakula na vivywaji vyao na walipewa mboga mboga tu.
Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.
17 Na kuhusu vijana hawa nne Mungu aliwapa uelewa na ufahamu katika maandiko yote na hekima, na Danieli aliweza kupambanua aina zote za maono na ndoto.
Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
18 Katika mwisho wa muda uliokuwa umepangwa na mfalme kuwaleta ndani, afisa mkuu aliwaleta mbele ya Nebukadneza.
Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza.
19 Mfalme aliongea nao, na miongoni mwa kundi lote hapo hapakuwa na wa kuwalinganisha na akina Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria. Walisimama mbele ya mfalme, wakiwa tayari kumtumikia.
Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme.
20 Katika kila swali la hekima na ufahamu ambalo mfalme aliwauliza, aliwakuta wakiwa na uwezo mara kumi kuliko waganga wote na wale waliojidai kusema na wafu, waliokuwa katika ufalme wake wote.
Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.
21 Danieli alikuwa hapo mpaka mwaka wa kwanza wa Mfalme Koreshi.
Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.

< Danieli 1 >