< 2 Samweli 15 >

1 Ikawa baada ya haya Absalomu akaandaa gari la farasi na farasi kwa ajili yake pamoja na watu hamsini wa kwenda mbele zake. 2 Absalomu alikuwa akiamka mapema na kusimama kando ya njia iliyoelekea katika lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na shauri la kuja kwa mfalme kwa ajili ya hukumu, Absalomu alimwita na kumwuliza, “Unatoka mji upi?” Na mtu yule hujibu, Mtumishi wako anatoka mojawapo ya kabila za Israeli.” 3 Hivyo Absalomu umwambia, “Tazama, shitaka lako ni jema na la haki, lakini hakuna aliyepewa mamlaka na mfalme kusikiliza shitaka lako. 4 Absalomu uongeza, “Natamani kwamba ningefanywa mwamzi ndani ya nchi ili kwamba kila mtu aliye na shitaka angeweza kuja kwangu nami ningempa haki. 5 Hivyo ikawa kila mtu aliyekuja kumweshimu Absalomu yeye hunyosha mkono na kumshika na kumbusu. 6 Absalomu alifanya hivi kwa Israeli wote waliokuja kwa mfalme kwa ajili ya hukumu. Hivyo Absalomu akaipotosha mioyo ya watu wa Israeli. 7 Ikawa mwishoni mwa miaka minne Absalomu akamwambia mfalme, “Tafadhari niruhusu niende ili nitimize nadhiri niliyoiweka kwa Yahwe huko Hebroni. 8 Kwa maana mtumishi wako aliweka nadhiri alipokuwako Geshuri katika Shamu akisema, 'Ikiwa Yahwe kweli atanirejesha Yerusalemu, ndipo nitamwabudu yeye.” 9 Hivyo mfalme akamwambia, “Nenda kwa amani”. Absalomu akainuka na kwenda Hebroni. 10 Kisha Absalomu akatuma wapelelezi katika jamaa zote za Israeli, kusema, “Mara msikiapo sauti ya tarumbeta semeni, 'Absalomu anatawala katika Hebroni.” 11 Watu mia mbili waliokuwa wamearikwa kutoka Yerusalemu wakaenda na Absalomu. Wakaenda katika ujinga wao bila kujua Absalomu alichokipanga. Wakati 12 Absalomu akitoa dhabihu, alituma watu kwa Ahithofeli katika mji wake huko Gilo. Yeye alikuwa mshauri wa Daudi. Uaini wa Absalomu ukawa na nguvu kwa kuwa watu waliomfuata waliendelea kuongezeka. 13 Mjumbe akaja kwa Daudi na kusema, “Mioyo ya watu wa Israeli inaambatana na Absalomu.” 14 Hivyo Daudi akawambia watumishi wake waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu, “Haya na tuinuke na kukimbia kwani hakuna hata mmoja atakayesalimika kwa Absalomu. Jiandaeni kuondoka mara moja asije akatupata mara hata akasababisha madhara juu yetu na kuushambulia mji kwa makali ya upanga.” 15 Watumishi wa mfalme wakamwambia, “Tazama, watumishi wako wapo tiyari kufanya lolote bwana wetu mfalme atakaloamua. 16 Mfalme akaondoka na familia yake yote pamoja naye, lakini mfalme akawaacha wanawake kumi waliokuwa masuria wa mfalme ili walitunze kasri. 17 Baada ya mfalme kwenda na watu wote pamoja naye, wakasimama katika nyumba ya mwisho. 18 Jeshi lake lote likaenda pamoja naye na mbele yake wakaenda Wakerethi na Wapelethi, na Wagiti mia sita wote waliokuwa wamemfuata kutoka Gathi. 19 Kisha mfalme akamwambia Itai Mgiti, “Kwa nini wewe pia uende nasi? Rudi na ukae na mfalme Absalomu kwa kuwa wewe ni mgeni tena mfungwa. Rudi mahali pako mwenyewe. 20 Kwani ni jana tu umeondoka, kwa nini nikufanye uzunguke nasi popote? Hata sijui niendako. Hivyo rudi pamoja na wenzako. Utiifu na uaminifu viambatane nawe.” 21 Lakini Itai akamjibu mfalme na kusema, “Kama Yahwe aishivyo na kama bwana wangu mfalme aishivyo, kwa hakika mahali popote bwana wangu mfalme aendako, mtumishi wako pia ndipo atakapokwenda, kwamba ni maisha au kifo.” 22 Hivyo Daudi akamwambia Itai, haya tangulia uende pamoja nasi.” Hivyo Itai Mgiti akaenda pamoja na mfalme, pamoja na watu wake wote na familia zao zote. 23 Nchi yote ikalia kwa sauti kadili watu walivyokuwa wakivuka Bonde la Kidroni, mfalme naye pia akavuka. Watu wote wakasafiri kuelekea nyikani. 24 Walikuwepo pia Sadoki pamoja na Walawi wote wamebeba sanduku la Mungu la agano. Wakaliweka sanduku la Mungu chini na kisha Abiathari akaungana nao. Wakasubiri mpaka watu wote walioondoka mjini walipokwisha kupita. 25 Mfalme akamwambia Sadoki, “Ulirudishe sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitaona neema machoni pa Yahwe atanirudisha na kunionesha tena sanduku na mahali likaapo. 26 Lakini ikiwa atasema, sipendezwi nawe,' tazama mimi nipo hapa, na anitendee yaliyo mema machoni pake.” 27 Pia mfalme akamwambia Sadoki kuhani, “Je wewe siyo mwonaji? Rudi mjini kwa amani na wanao wawili, Ahimaazi mwanao na Yonathani mwana wa Abiathari. 28 Tazama nitasubiri katika vivuko vya Araba mpaka nitakapo pata neno kutoka kwenu kunitaarifu.” 29 Hivyo Sadoki na Abiathari wakalirudish sanduku la Mungu Yerusalemu nao wakakaa humo. 30 Lakini Daudi akaenda bila viatu huku akilia hata Mlima wa Mizeituni, naye alikuwa amefunika kichwa chake. Kila mtu miongoni mwao waliokuwa pamoja naye akafunika kichwa chake, nao wakaenda huku wakilia. 31 Mtu mmoja akamwambia Daudi kusema, Ahithofeli ni miongoni mwa waaini walio pamoja na Absalomu.” Hivyo Daudi akaomba, “Ee Yahwe, tafadhari badili ushauri wa Ahithofeli kuwa upumbavu.” 32 Ikawa Daudi alipofika juu njiani mahala Mungu alipokuwa akiabudiwa, Hushai Mwarki akaja kumlaki vazi lake limeraruliwa na mavumbi kichwani pake. 33 Daudi akamwambia, “Ikiwa utaenda nami utakuwa mzigo kwangu. 34 Lakini ukirudi mjini na kumwambia Absalomu, 'Nitakuwa mtumishi wa mfalme kama nilivokuwa mtumishi wa baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako,' ndipo utayageuza mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu. 35 Je haunao pamoja nawe Sadoki na Abiathari makuhani? Hivyo chochote ukisikiacho katika kasri, uwaambie Sadoki na Abiathari makuhani. 36 Tazama wanao pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani mwana wa Abiathari. Mniletee habari juu ya kila mnachokisikia.” 37 Hivyo Hushai, rafiki wa Daudi, akaja mjini wakati Absalomu anafika na kuingia Yerusalemu.

< 2 Samweli 15 >