< 2 Wakorintho 9 >

1 Kuhusiana na huduma kwa ajili ya waumini, ni bora zaidi kwangu kuwaandikia. 2 Ninajua kuhusu shauku yenu, ambayo nilijivunia kwa watu wa Makedonia. Niliwaambia kwamba Akaya imekuwa tayari tangu mwaka uliopita. Hamu yenu imewatia moyo wengi wao kutenda. 3 Sasa, nimewatuma ndugu ili kwamba majivuno yetu kuhusu ninyi yasiwe ya bure, na ili kwamba mngekuwa tayari, kama nilivyosema mngekuwa. 4 Vinginevyo, kama mtu yeyote wa Makedonia akija pamoja nami na kuwakuta hamjawa tayari, tungeona haya — sisemi chochote kuhusu ninyi—kwa kuwa jasiri sana katika ninyi. 5 Hivyo niliona ilikuwa muhimu kuwasihi ndugu kuja kwenu na kufanya mipango mapema kwa ajili ya zawadi mlizoahidi. Hii ni hivyo ili kwamba ziwe tayari kama baraka, na si kama kitu kilichoamriwa. 6 Wazo ni hili: mtu apandaye haba pia atavuna haba, na yeyote apandaye kwa lengo la baraka pia atavuna baraka. 7 Basi na kila mmoja atoe kama alivyopanga moyoni mwake. Basi naye asitoe kwa huzuni au kwa kulazimishwa. Kwa kuwa Mungu humpenda yule atoaye kwa furaha. 8 Na Mungu anaweza kuizidishia kila baraka kwa ajili yenu, ili kwamba, kila wakati, katika mambo yote, muweze kupata yote mnayohitaji. Hii itakuwa ili kwamba mueze kuzidisha kila tendo jema. 9 Ni kama ilivyoandikwa: “Ametapanya utajiri wake na kuutoa kwa maskini. Haki yake yadumu milele.” (aiōn g165) 10 Naye atoaye mbegu kwa mpanzi na mkate kwa ajili ya chakula, pia atatoa na kuzidisha mbegu yenu kwa ajili ya kupanda. Yeye ataongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili kwamba muweze kuwa wakarimu. Hii italeta shukrani kwa Mungu kupitia sisi. 12 Kwa kufanya huduma hii sio tu inagusa mahitaji ya waumini. Pia huzidisha katika matendo mengi ya shukrani kwa Mungu. 13 Kwa sababu ya kupimwa kwenu na kuthibitishwa kwa huduma hii, pia mtamtukuza Mungu kwa utii kwa ukiri wenu wa injili ya Kristo. Pia mtamtukuza Mungu kwa ukarimu wa karama yenu kwao na kwa kila mmoja. 14 Wanawatamani, na wanaomba kwa ajili yenu. Wanafanya hivi kwa sababu ya neema kubwa ya Mungu iliyo juu yenu. 15 Shukrani ziwe kwa Mungu kwa karama yake isiyoelezeka!

< 2 Wakorintho 9 >