< 1 Samweli 15 >

1 Samweli akamwambia Sauli, “BWANA alinituma nikutie mafuta uwe mfalme wa watu wake Israeli. Basi sikiliza maneno ya BWANA. 2 Hivi ndivyo BWANA wa majeshi asemavyo, 'Nilichunguza jinsi Amaleki alivyomfanyia Israeli kwa kuwapinga njiani, walipopanda kutoka Misri. 3 Sasa nenda umshambulie Amaleki na ukaangamize kabisa vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache, ua wote mwanamme na mwanamke, mtoto na mtoto mchanga, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.”' 4 Sauli akwaita watu na kuwahesabu katika mji wa Talemu: watu mia mbili elfu waendao kwa miguu, na watu elfu kumi kutoka Yuda. 5 Kisha Sauli akaja hadi mji wa Amaleki akangoja huko bondeni. 6 Ndipo Sauli akawaambia Wakeni, “Nendeni, muondoke, mkajitenge na Waamaleki, nisije kuwaangamiza pamoja nao. Kwa maana ulionesha wema kwa watu wote wa Israeli, walipotoka Misri.” Kwa hiyo Wakeni wakajitenga na Waamaleki. 7 Kisha sauli akawashambulia Waamaleki, kutoka Havila hadi kufika Shuri, ulio mashariki mwa Misri. 8 Basi akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai; aliwaangamiza kabisa watu wote kwa ncha ya upanga. 9 Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi akiwa hai, pamoja na kondoo wazuri, ng'ombe, ndama wanono, na wanakondoo. Kila kitu kilichokuwa kizuri, hawakukiangamiza. Bali waliangamiza kabisa chochote kilichodharaulika na kisicho na thamani. 10 Baadaye neno la BWANA likamjia Samweli, kusema, 11 “Inanihuzunisha kwamba nimemchagua Samweli awe mfalme, kwa maana aligeuka nyuma asinifuate na hakutekeleza maagizo yangu.” Samweli alikasirika; akamlilia BWANA usiku kucha. 12 Samweli aliamka mapema akutane na Sauli wakati wa asubuhi. Samweli aliambiwa, “Sauli alifika Karmeli na amejijengea ukumbusho kwa ajili yake, kisha aligeuka na kuendelea chini hadi Gilgali.” Ndipo 13 Samweli akamwendea Sauli, na Sauli akamwambia, “Umebarikiwa na BWANA! Nami nimetekeleza amri ya BWANA.” 14 Samweli akasema, “Hicho kilio cha kondoo ni cha nini basi masikioni mwangu, na hiyo milio ya ng'ombe ninayosikia? 15 Sauli akamjibu, “Wao wamewaleta kutoka kwa Waamaleki. Kwa sababu watu waliwaacha hai kondoo wazuri na ng'ombe, kwa ajili ya sadaka kwa BWANA Mungu wako. Zilizobaki tuliziangamiza kabisa.” 16 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, “Subiri nitakumbia kile ambacho BWANA amekisema kwangu usiku.” Sauli akamwambia, “Sema!” 17 Samweli akasema, “Ingawa wewe ni mdogo machoni pako mwenyewe, je, hukufanywa mkuu wa kabila za Israeli? Na BWANA akakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli; 18 BWANA alikutuma katika safari yako akisema, 'nenda na uangamize kabisa wenye dhambi, Waamaleki, na upigane dhidi yao hadi wameangamizwa.' 19 Kwa nini basi haukuitii sauti ya BWANA, bali badala yake ulishikilia nyara na ukafanya uovu machoni pa BWANA?” 20 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Kweli kabisa niliitii sauti ya BWANA, Na nimeifuata njia ambayo BWANA alinituma. Nimemteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, na kuwaangamiza kabisa Waamaleki. 21 Lakini watu walichukua baadhi ya nyara-kondoo na ng'ombe, na vitu vizuri vilivyokusudiwa kuangamizwa, ili wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.” 22 Samweli akajibu, “Je, BWANA hufurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama ilivyo kuitii sauti yake? Utii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia ni bora kuliko mafuta ya beberu. 23 Kwa maana uasi ni sawa na dhambi ya uchawi, na ukaidi ni sawa na uovu na udhalimu. Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, naye pia amekukataa usiwe mfalme.” 24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi; kwa maana nimevunja amri ya BWANA na maneno yako, kwa sababu niliwaogopa watu na kuitii sauti yao. 25 Sasa, tafadhali nisamehe dhambi yangu, na urudi nami ili nipate kumcha BWANA.” 26 Samweli akamwambia Sauli, “Sitarudi pamoja na wewe; kwa sababu umekataa neno la BWANA, naye BWANA amekukataa usiwe mfalme juu ya Israeli.” 27 Samweli alipogeuka kuondoka, Sauli akashika pindo la kanzu yake, na likachanika. 28 Samweli akamwambia, “BWANA ameuchana ufalme wa Israeli kutoka kwako leo na amempa ufalme huo jirani yako, aliye bora kuliko wewe. 29 Pia, yeye ni Uwezo wa Israeli hatasema uongo wala kubadili nia yake; kwa sababu si mwanadamu, kwamba abadili nia yake.” 30 Kisha Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali nipe heshima wakati huu mbele ya wakuu wa watu wangu na mbele ya Israeli. Urudi tena pamoja nami, kusudi niweze kumcha BWANA, Mungu wako.” 31 Hivyo Samweli akamrudia tena Sauli, na Sauli akamcha BWANA. 32 Kisha Samweli akasema, “Mmlete hapa kwangu Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akafika kwake akiwa amefungwa minyororo na kusema, “Hakika uchungu wa kifo umepita.” 33 Naye Samweli akamjibu, “Jinsi upanga wako ulivyofanya wanawake wapoteze watoto, vivyo hivyo mama yako naye hatakuwa na mtoto miongoni mwa wanawake.” Kisha Samweli akamkata Agagi vipande vipande mbele za BWANA huko Gilgali. 34 Samweli akaenda Rama, na Sauli akapanda kwenda nyumbani kwake Gibea ya Sauli. 35 Samweli hakumuona tena Sauli hadi siku ya kifo chake, lakini alimwombolezea Sauli. Na BWANA alijuta kwa kumfanya Sauli awe mfalme juu ya Israeli.

< 1 Samweli 15 >