< 1 Samweli 1 >

1 Palikuwa na mtu mmoja wa Rama Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu; jina lake aliitwa Elikana mwana Yerohamu mwana Elihu mwana wa Tohu mwana wa Sufu, Mwefraimu. 2 Mtu huyo alioa wanawake wawili, jina la mke wa kwanza aliitwa Hana, na yule wa pili aliitwa Penina, Penina alizaa watoto, lakini Hana hakuzaa. 3 Kila mwaka, mtu huyu aliondoka mjini kwake kwenda kuabudu na kutoa dhabihu kwa BWANA wa majeshi huko Shilo. Wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa BWANA, walikuwepo huko Shilo. 4 Kila mwaka zamu ya Elikana ya kutoa dhabihu ilipofika, alikuwa daima akimpa sehemu ya nyama Penina mkewe, watoto wake wote wa kiume na wakike 5 Lakini kwa mgawo wa Hana daima alimpa mara mbili zaidi, kwa sababu alimpenda Hana, ingawa BWANA alikuwa amelifunga tumbo lake. 6 Hasimu wake alimchokoza sana ili kumkasilisha, kwa sababu BWANA alikuwa amelifunga tumbo lake. 8 7 Hivyo kila mwaka, alipokuwa akienda katika nyumba ya BWANA pamoja na familia yake, hasimu wake alizidi kumchokoza, Hatimaye alikuwa mtu wa kulia kila wakati na hakula kitu chochote. 8 Elikana mmewe kila wakati alimuuliza, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli chakula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Mimi sibora kwako kuliko wana kumi? 9 Wakati fulani, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alinyanyuka. Wakati huo Eli, kuhani alikuwa amekaa juu ya kiti chake mlangoni kuelekea nyumba ya BWANA. 10 Hana alijawa na uchungu sana; akamwomba BWANA na akalia mno. 11 Aliweka nadhili na kusema, “BWANA wa majeshi, kama utalitazama teso la mjakazi wako na kunikumbuka, na usipomsahau mjakazi wako, na kumpatia mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo nitamtoa huyo mtoto kwa BWANA siku zote za maisha yake, na wembe hautapita juu ya kichwa chake kamwe”. 12 Hana kiendelea kuomba mbele za BWANA, Eli alikitazama kinywa chake. 13 Hana aliongea moyoni mwake. Midomo yake ilitikisika, lakini sauti yake haikusikika. Hivyo Eli alimdhania kuwa amelewa. 14 Eli akamwambia, “Utakuwa mlevi mpaka lini? Weka mbali divai yako.” 15 Hana akajibu, “Sivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni. Sijanywa divai wala kinywaji chochote cha kulevya, bali nimekuwa nikiimimina nafsi yangu mbele za BWANA.” 16 Usimchukulie mjakazi wako kama mwanamke duni; nimekuwa nikiongea kutokana na maumivu na masikitiko yangu.” 18 17 Kisha Eli alimjibu na kusema, “Nenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akupatie kile ulichomuomba.” 18 Hana akasema, “Na mjakazi wako apate kibali machoni pako.” Ndipo huyo mwanamke alienda zake na kula chakula na hakuhuzunika tena. 19 Waliamka asubuhi na mapema wakaenda wakamtukuza BWANA, na baadaye walirudi nyumbani kwao Rama. Elikana alilala na mke wake Hana, na BWANA akamkumbuka. 20 Baada ya muda fulani, Hana alibeba mimba na akazaa mtoto wa kiume. Akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa sababu huyu nilimuomba kutoka kwa BWANA.” 21 Mara nyingine, Elikana na nyumba yake, walipanda kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya Mwaka na kuondoa nadhiri yake. 22 Lakini Hana hakwenda huko; alikuwa amekwisha mwambia mmewe, “Sitaenda huko hadi mtoto aache kunyonya; ndipo nitamleta, ili ahudhurie mbele za BWANA na akae huko daima.” 23 Mme wake Hana, Elikana, akamwambia, “Fanya yale yakupendezayo. Ngojea hadi utakapokuwa umemwachisha kunyonya; BWANA aweze peke yake kuthibitisha neno lake.” Hivyo yule mwanamke alibaki akimnyonyesha mtoto wake mpaka pale alipomwachisha ziwa. 24 Alipokuwa amemwachisha kunyonya, alimbeba, akimchukua pamoja ng'ombe dume wa miaka mitatu, unga kama kilo thelathini na chupa ya mvinyo, akampeleka katika nyumba ya BWANA huko Shilo. Na mtoto huyo alikuwa bado mdogo. 25 Walimchinja yule ng'ombe, na wakamkabidhi mtoto kwa Eli. 26 Akasema, “Ee bwana wangu! Kama uishivyo, bwana wangu, Mimi ndiye yule mwanamke niliyesimama hapa karibu nawe nikimwomba BWANA. 27 Niliomba kwa ajili ya mtoto huyu na BWANA akawa amenijibu ombi la dua yangu nililomwomba. 28 Nami nimemtoa kwa BWANA; kwa maisha yake yote, nimempa BWANA.” Ndipo Elikana na familia yake wakamtukuza BWANA huko Shilo.

< 1 Samweli 1 >