< 1 Wafalme 5 >

1 Hiramu mfalme wa Tiro aliwatuma watumishi wake kwa Sulemani kwa kuwa alisikia kuwa walikuwa wamemtawaza kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwani Hiramu alimpenda Daudi. 2 Sulemani akatuma ujumbe kwa Hiramu, akisema, 3 “Unajua kuwa Daudi baba yangu hakujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wake kwa sababu ya vile vita vilivyomzunguka, kwa kuwa wakati wa uhai wake BWANA alikuwa akiweka maadui wake chini ya nyayo za miguu yake. 4 Lakini sasa BWANA amenipa mimi pumziko toka pande zote. Hakuna maadui wala majanga. 5 Kwa hiyo ninakusudia kujenga hekalu kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyosema kwa Daudi baba yangu, akisema, 'Mwanao ambaye nitamweka kwenye kiti chako cha enzi mahali pako, ndiye atakayenijengea hekalu kwa jina langu.' 6 Kwa hiyo sasa amuru wakate mierezi kutoka Lebanoni kwa ajili yangu. Watumishi wangu wataungana na watumishi wako, nami nitakulipa kwa ajili ya watumishi wako ili kwamba upate malipo mazuri kwa kila kitu utakchokubali kukifanya. Kwa kuwa unajua kuwa hakuna mtu mioingoni mwetu anayejua kukata miti kama Wasidoni.” 7 Hiramu aliposikia maneno ya Sulemani, akafurahi sana akasema, “BWANA na abarikiwe leo, ambaye amempa Daudi mwana wa hekiima juu ya kundi hili kubwa.” 8 Hiramu akatuma neno kwa Sulemani, akisema, “Nimeupata ujumbe ule ulionitumia. Nitatoa miti yote ya mierezi na miti ya miberoshi ambayo unahitaji. 9 Watumishi wangu wataileta miti kutoka Lebanoni hadi baharini, nami nitaiendesha baharini mpaka mahali utakaponielekeza. Nitaigawa pale, nawe utaichukua. Utafanya kile ninachohitaji kwa kuwapa chakula watumishi wangu.” 10 Kwa hiyo Hiramu akampa Sulemani miti yote ya mierezi na miti ya miberoshi ambayo alihitaji. 11 Sulemani akampa Hiramu kori ishirini elfu za ngano kwa ajili ya chakula cha watumishi wake na kori ishirii za mafuta safi. Sulemani akavitoa hivi kwa Hiramu mwaka baad ya mwaka. 12 BWANA akampa Sulemani hekima, kama alivyokuwa amemwahidi. Kulikuwa na amani kati ya Hiramu na Sulemani na wote wawili wakafanya agano. 13 Mfalme Sulemani akaandaa wafanya kazi kutoka Israeli yote. Idadi ya watenda kazi walioandaliwa ilikuwa wanaume elfu thelathini. 14 Aliwatuma kwenda Lebanoni, aliwatuma kwa zamu ya watu elfu kumi kila mwezi. Kwa mwezi mmoja walienda Lebanoni na miezi miwili walikaa nyumbani. Adoniramu ndiye aliyekuwa msimamizi wa watenda kazi. 15 Sulemani alikuwa na watu elfu sabini waliokuwa wabeba mizigo na watu elfu themanini wa kukata mawe milimani, 16 zaidi ya hao, walikuwepo maakida 3, 300 ambao pia waliokuwa wakiisimamia hiyo kazi. 17 Kwa amri ya mfalme walileta mawe makubwa ya thamani kwa ajili ya kulaza kwenye msingi wa hekalu. 18 Kwa hiyo wajenzi wa Sulemani na wajenzi wa Hiramu na Wagebaliti walifanya kazi ya kukata na kuandaa mbao kwa ajili ya ujenzi wa hekalu.

< 1 Wafalme 5 >