< 1 Wakorintho 1 >

1 Paulo, aliyeitwa na Kristo Yesu kuwa mtume kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, 2 kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale ambao wamewekwa wakfu katika Yesu Kristo, ambao wameitwa kuwa watu watakatifu. Tunawaandikia pia wale wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo katika mahali pote, Bwana wao na wetu. 3 Neema na amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo. 4 Siku zote namshukru Mungu wangu kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu ambayo Kristo Yesu aliwapa. 5 Amewafanya kuwa matajiri katika kila njia, katika usemi na pamoja maarifa yote. 6 Amewafanya matajiri, kama ushuhuda kuhusu Kristo ya kwamba amethibitishwa kuwa kweli miongoni mwenu. 7 Kwa hiyo hampungukiwi karama za kiroho, kama mlivyo na hamu ya kusubiri ufunuo wa Bwana wetu Yesu Kristo. 8 Atawaimarisha ninyi pia hadi mwisho, ili msilaumiwe siku ya Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Mungu ni mwaminifu ambaye aliwaita ninyi katika ushirika wa mwana wake, Yesu Kristo Bwana wetu. 10 Sasa nawasihi kaka na dada zangu, kupitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba wote mkubali, na kwamba kusiwe na migawanyiko miongoni mwenu. Nawasihi kwamba muungane pamoja katika nia moja na katika kusudi moja. 11 Kwani watu wa nyumba ya Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mgawanyiko unaoendelea miongoni mwenu. 12 Nina maana hii: Kila mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo,” au “Mimi ni wa Apolo”, au “Mimi ni wa Kefa” au “Mimi ni wa Kristo”. 13 Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14 Namshukuru Mungu kuwa sikumbatiza yeyote, isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Hii ilikuwa kwamba hakuna yeyote angesema mlibatizwa kwa jina langu. 16 (Pia niliwabatiza wa nyumba ya Stephania. Zaidi ya hapo, sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote). 17 Kwa kuwa, Kristo hakunituma kubatiza bali kuhubiri injili. Hakunituma kuhubiri kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili kwamba nguvu ya msalaba wa Kristo isiondolewe. 18 Kwa kuwa ujumbe wa msalaba ni upuuzi kwa wale wanaokufa. Lakini kwa wale ambao Mungu anawaokoa, ni nguvu ya Mungu. 19 Kwa kuwa imeandikwa, “Nitaiharibu hekima ya wenye busara. Nitauharibu ufahamu wa wenye akili.” 20 Yuko wapi mtu mwenye busara? Yuko wapi mwenye elimu? Yuko wapi msemaji mshawishi wa dunia hii? Je, Mungu hakuigeuza hekima ya dunia hii kuwa ujinga? (aiōn g165) 21 Tangu dunia imekuwa katika hekima yake haikumjua Mungu, ilimpendeza Mungu katika ujinga wao wa kuhubiri ili kuokoa wale wanaoamini. 22 Kwa Wayahudi huuliza ishara za miujiza na kwa Wayunani hutafuta hekima. 23 Lakini tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa, aliye kikwazo kwa Wayahudi na ni ujinga kwa Wayunani. 24 Lakini kwa wale ambao waliitwa na Mungu, Wayahudi na Wayunani, tunamhubiri Kristo kama nguvu na hekima ya Mungu. 25 Kwa kuwa ujinga wa Mungu una hekima kuliko ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. 26 Angalia wito wa Mungu juu yenu, kaka na dada zangu. Si wengi wenu mlikuwa na hekima katika viwango vya kibinadamu. Si wengi wenu mlikuwa na nguvu. Si wengi wenu mlizaliwa katika ukuu. 27 Lakini Mungu alichagua vitu vijinga vya dunia ili kuviaibisha vyenye hekima. Mungu alichagua kilicho dhaifu katika dunia kukiaibisha chenye nguvu. 28 Mungu alichagua kile kilicho cha hali ya chini na kilichodharauliwa katika dunia. Alichagua hata vitu ambavyo havikuhesabiwa kuwa kitu, kwa kuvifanya si kitu vitu vilivyo na thamani. 29 Alifanya hivi ili asiwepo yeyote aliye na sababu ya kujivuna mbele zake. 30 Kwa sababu ya kile Mungu alichofanya, sasa mko ndani ya Kristo Yesu, ambaye amefanyika hekima kwa ajili yetu kutoka kwa Mungu. Alikuwa haki yetu, utakatifu na ukombozi. 31 Kama matokeo, kama andiko lisemavyo, “Anayejisifu, ajisifu katika Bwana.”

< 1 Wakorintho 1 >