< Zaburi 1 >

1 Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha. 2 Bali huifurahia sheria ya Bwana, naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana. 3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa. 4 Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. 5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki. 6 Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki, bali njia ya waovu itaangamia.

< Zaburi 1 >