< Zaburi 67 >

1 Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo. Mungu aturehemu na kutubariki, na kutuangazia nuru za uso wake, 2 ili njia zako zijulikane duniani, wokovu wako katikati ya mataifa yote. 3 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu. 4 Mataifa yote wafurahi na kuimba kwa shangwe, kwa kuwa unatawala watu kwa haki na kuongoza mataifa ya dunia. 5 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu. 6 Ndipo nchi itatoa mazao yake, naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki. 7 Mungu atatubariki na miisho yote ya dunia itamcha yeye.

< Zaburi 67 >