< Zaburi 64 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui. 2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu, kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya. 3 Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha. 4 Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga. 5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza juu ya kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?” 6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila. 7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa. 8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau. 9 Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda. 10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

< Zaburi 64 >