< Zaburi 61 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, sikia kilio changu, usikilize maombi yangu. 2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita, ninaita huku moyo wangu unadhoofika; uniongoze kwenye mwamba ule ulio juu kuliko mimi. 3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu, ngome imara dhidi ya adui. 4 Natamani kukaa hemani mwako milele, na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako. 5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu, umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako. 6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake, miaka yake kwa vizazi vingi. 7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele; amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde. 8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.

< Zaburi 61 >