< Zaburi 29 >

1 Zaburi ya Daudi. Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu. 2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake. 3 Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu. 4 Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu. 5 Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. 6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. 7 Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi. 8 Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi. 9 Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” 10 Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele. 11 Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.

< Zaburi 29 >