< Zaburi 28 >

1 Zaburi ya Daudi. Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu; usiwe kwangu kama kiziwi. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni. 2 Sikia kilio changu unihurumie ninapokuita kwa ajili ya msaada, niinuapo mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako. 3 Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki. 4 Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili. 5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena. 6 Bwana asifiwe, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie. 7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo. 8 Bwana ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake. 9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

< Zaburi 28 >