< Zaburi 20 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki, jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako. 2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu na akupatie msaada kutoka Sayuni. 3 Na azikumbuke dhabihu zako zote, na azikubali sadaka zako za kuteketezwa. 4 Na akujalie haja ya moyo wako, na aifanikishe mipango yako yote. 5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. Bwana na akupe haja zako zote. 6 Sasa nafahamu kuwa Bwana humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume. 7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu. 8 Wao wameshushwa chini na kuanguka, bali sisi tunainuka na kusimama imara. 9 Ee Bwana, mwokoe mfalme! Tujibu tunapokuita!

< Zaburi 20 >