< Zaburi 142 >

1 Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi. Namlilia Bwana kwa sauti, nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie. 2 Namimina malalamiko yangu mbele zake, mbele zake naeleza shida zangu. 3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu, wewe ndiwe unajua njia zangu. Katika njia ninayopita watu wameniwekea mtego. 4 Tazama kuume kwangu na uone, hakuna hata mmoja anayejihusisha nami. Sina kimbilio, hakuna anayejali maisha yangu. 5 Ee Bwana, nakulilia wewe, nasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai.” 6 Sikiliza kilio changu, kwa sababu mimi ni mhitaji sana; niokoe na wale wanaonifuatilia, kwa kuwa wamenizidi nguvu. 7 Nifungue kutoka kifungo changu, ili niweze kulisifu jina lako. Ndipo wenye haki watanizunguka, kwa sababu ya wema wako kwangu.

< Zaburi 142 >