< Zaburi 141 >

1 Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita. 2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni. 3 Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu. 4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa. 5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda mabaya, 6 watawala wao watatupwa chini kutoka kwenye majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli. 7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.” (Sheol h7585) 8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife. 9 Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya. 10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.

< Zaburi 141 >