< Hesabu 26 >

1 Baada ya hiyo tauni, Bwana akamwambia Mose na Eleazari mwana wa kuhani Aroni, 2 “Hesabu jumuiya yote ya Kiisraeli kwa jamaa zao, wale wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, ambao wanaweza kutumika katika jeshi la Israeli.” 3 Hivyo Mose na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare ya Moabu, ngʼambo ya Yordani kutokea Yeriko, wakasema, 4 “Hesabuni wanaume wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.” Hawa ndio Waisraeli waliotoka Misri: 5 Wazao wa Reubeni, mwana mzaliwa wa kwanza wa Israeli, walikuwa: kutoka kwa Hanoki, ukoo wa Wahanoki; kutoka kwa Palu, ukoo wa Wapalu; 6 kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Karmi, ukoo wa Wakarmi. 7 Hizi zilikuwa ndizo koo za Reubeni; wale waliohesabiwa walikuwa 43,730. 8 Mwana wa Palu alikuwa Eliabu, 9 nao wana wa Eliabu walikuwa Nemueli, Dathani na Abiramu. Hawa wawili Dathani na Abiramu ndio walikuwa maafisa wa jumuiya ambao walimwasi Mose na Aroni, na walikuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora wakati walimwasi Bwana. 10 Ardhi ilifunua kinywa chake na kuwameza pamoja na Kora, ambaye wafuasi wake walikufa wakati moto ulipowateketeza wanaume 250. Nao walikuwa kama alama ya onyo. 11 Pamoja na hayo, hao ukoo wa Kora hawakufa. 12 Wazao wa Simeoni kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Nemueli, ukoo wa Wanemueli; kutoka kwa Yamini, ukoo wa Wayamini; kutoka wa Yakini, ukoo wa Wayakini; 13 kutoka kwa Zera, ukoo wa Wazera; kutoka kwa Shauli, ukoo wa Washauli. 14 Hizi ndizo koo za Simeoni; walikuwa 22,200. 15 Wazao wa Gadi kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Sifoni, ukoo wa Wasifoni; kutoka kwa Hagi, ukoo wa Wahagi; kutoka kwa Shuni, ukoo wa Washuni; 16 kutoka kwa Ozni, ukoo wa Waozni; kutoka kwa Eri, ukoo wa Waeri; 17 kutoka kwa Arodi, ukoo wa Waarodi; kutoka kwa Areli, ukoo wa Waareli. 18 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Gadi; wale waliohesabiwa walikuwa 40,500. 19 Eri na Onani walikuwa wana wa Yuda, lakini walifia huko Kanaani. 20 Wazao wa Yuda kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Shela, ukoo wa Washela; kutoka kwa Peresi, ukoo wa Waperesi; kutoka kwa Zera, ukoo wa Wazera. 21 Wazao wa Peresi walikuwa: kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Hamuli, ukoo wa Wahamuli. 22 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Yuda; wale waliohesabiwa walikuwa 76,500. 23 Wazao wa Isakari kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Tola, ukoo wa Watola; kutoka kwa Puva, ukoo wa Wapuva; 24 kutoka kwa Yashubu, ukoo wa Wayashubu; kutoka kwa Shimroni, ukoo wa Washimroni. 25 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Isakari; wale waliohesabiwa walikuwa 64,300. 26 Wazao wa Zabuloni kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Seredi, ukoo wa Waseredi; kutoka kwa Eloni, ukoo wa Waeloni; kutoka kwa Yaleeli, ukoo wa Wayaleeli. 27 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Zabuloni, wale waliohesabiwa walikuwa 60,500. 28 Wazao wa Yosefu kwa koo zao kutoka kwa Manase na kwa Efraimu walikuwa: 29 Wazao wa Manase: kutoka kwa Makiri, ukoo wa Wamakiri (Makiri alikuwa baba wa Gileadi); kutoka kwa Gileadi, ukoo wa Wagileadi. 30 Hawa ndio waliokuwa wazao wa Gileadi: kutoka kwa Iezeri, ukoo wa Waiezeri; kutoka kwa Heleki, ukoo wa Waheleki; 31 kutoka kwa Asirieli, ukoo wa Waasirieli; kutoka kwa Shekemu, ukoo wa Washekemu; 32 kutoka kwa Shemida, ukoo wa Washemida; kutoka kwa Heferi, ukoo wa Waheferi. 33 (Selofehadi mwana wa Heferi hakuzaa wana, bali alikuwa na watoto wa kike tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.) 34 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Manase; wale waliohesabiwa walikuwa 52,700. 35 Hawa walikuwa wazao wa Efraimu kwa koo zao: kutoka kwa Shuthela, ukoo wa Washuthela; kutoka kwa Bekeri, ukoo wa Wabekeri; kutoka kwa Tahani, ukoo wa Watahani; 36 Hawa ndio walikuwa wazao wa Shuthela: kutoka kwa Erani, ukoo wa Waerani. 37 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Efraimu; wale waliohesabiwa walikuwa 32,500. Hawa ndio waliokuwa wazao wa Yosefu kwa koo zao. 38 Wazao wa Benyamini kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Bela, ukoo wa Wabela; kutoka kwa Ashbeli, ukoo wa Waashbeli; kutoka kwa Ahiramu, ukoo wa Waahiramu; 39 kutoka kwa Shufamu, ukoo wa Washufamu; kutoka kwa Hufamu, ukoo wa Wahufamu. 40 Wazao wa Bela kutoka kwa Ardi na Naamani walikuwa: kutoka kwa Ardi, ukoo wa Waardi; kutoka kwa Naamani, ukoo wa Wanaamani. 41 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Benyamini; wale waliohesabiwa walikuwa 45,600. 42 Hawa ndio waliokuwa wazao wa Dani kwa koo zao: kutoka kwa Shuhamu, ukoo wa Washuhamu. Hizi ndizo zilizokuwa koo za Dani: 43 Wote walikuwa koo za Washuhamu; wale waliohesabiwa walikuwa 64,400. 44 Wazao wa Asheri kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Imna, ukoo wa Waimna; kutoka kwa Ishvi, ukoo wa Waishvi; kutoka kwa Beria, ukoo wa Waberia; 45 kutoka kwa wazao wa Beria: kutoka kwa Heberi, ukoo wa Waheberi; kutoka kwa Malkieli, ukoo wa Wamalkieli. 46 (Asheri alikuwa na binti aliyeitwa Sera.) 47 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Asheri; wale waliohesabiwa walikuwa 53,400. 48 Wazao wa Naftali kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Yaseeli, ukoo wa Wayaseeli; kutoka kwa Guni, ukoo wa Waguni; 49 kutoka kwa Yeseri, ukoo wa Wayeseri; kutoka kwa Shilemu, ukoo wa Washilemu. 50 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Naftali; wale waliohesabiwa walikuwa 45,400. 51 Jumla ya hesabu ya wanaume wa Israeli ilikuwa 601,730. 52 Bwana akamwambia Mose, 53 “Watagawiwa nchi kama urithi kwa kulingana na hesabu ya majina. 54 Kundi kubwa zaidi lipe urithi mkubwa zaidi, na kundi dogo zaidi lipewe urithi mdogo zaidi; kila kundi litapokea urithi wake kulingana na hesabu ya wale walioorodheshwa. 55 Hakikisha kuwa nchi inagawanywa kwa kura. Kile kitakachorithiwa na kila kikundi kitakuwa kwa kulingana na majina ya kabila la babu yao. 56 Kila urithi utagawanywa kwa kura miongoni mwa makundi makubwa na madogo.” 57 Hawa walikuwa Walawi ambao walihesabiwa kwa koo zao: kutoka kwa Gershoni, ukoo wa Wagershoni; kutoka kwa Kohathi, ukoo wa Wakohathi; kutoka kwa Merari, ukoo wa Wamerari. 58 Hizi pia zilikuwa koo za Walawi: ukoo wa Walibni; ukoo wa Wahebroni; ukoo wa Wamahli; ukoo wa Wamushi; ukoo wa wana wa Kora. (Kohathi alikuwa baba aliyemzaa Amramu; 59 jina la mke wa Amramu ni Yokebedi, naye pia alikuwa mzao wa Lawi, ambaye alizaliwa kwa Walawi nchini Misri. Alimzalia Amramu: Aroni, Mose na dada yao Miriamu. 60 Aroni alikuwa baba yake Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari. 61 Lakini Nadabu na Abihu walikufa wakati walitoa sadaka mbele za Bwana kwa moto usioruhusiwa.) 62 Wanaume wote wa Walawi wa umri wa mwezi mmoja na zaidi walikuwa 23,000. Wao hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine kwa sababu hawakupokea urithi miongoni mwao. 63 Hawa ndio walioorodheshwa na Mose na kuhani Eleazari wakati waliwahesabu Waisraeli kwenye nchi tambarare ya Moabu, kando ya Yordani ngʼambo ya Yeriko. 64 Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa miongoni mwa wale waliohesabiwa na Mose na kuhani Aroni wakati waliwahesabu Waisraeli katika Jangwa la Sinai. 65 Kwa maana Bwana alikuwa amewaambia hao Waisraeli hakika wangekufa huko jangwani, wala hakuna mmoja wao aliyeachwa, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni.

< Hesabu 26 >