< Luka 3 >

1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene, 2 nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko jangwani. 3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake. 5 Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitashushwa. Njia zilizopinda zitanyooshwa, na zilizoparuza zitasawazishwa. 6 Nao watu wote watauona wokovu wa Mungu.’” 7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya. 9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” 10 Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?” 11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.” 12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?” 13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.” 14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.” 15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo. 16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” 18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema. 19 Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, 20 Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yohana gerezani. 21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. 22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.” 23 Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Eli, 24 Eli alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, Lawi alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Yanai, Yanai alikuwa mwana wa Yosefu, 25 Yosefu alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Amosi, Amosi alikuwa mwana wa Nahumu, Nahumu alikuwa mwana wa Esli, Esli alikuwa mwana wa Nagai, 26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi, Maathi alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Semeini, Semeini alikuwa mwana wa Yoseki, Yoseki alikuwa mwana wa Yoda, 27 Yoda alikuwa mwana wa Yoanani, Yoanani alikuwa mwana wa Resa, Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli, Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli, Shealtieli alikuwa mwana wa Neri, 28 Neri alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Adi, Adi alikuwa mwana wa Kosamu, Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu, Elmadamu alikuwa mwana wa Eri, 29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua, Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri, Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu, Yorimu alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, 30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni, Simeoni alikuwa mwana wa Yuda, Yuda alikuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Yonamu, Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu, Eliakimu alikuwa mwana wa Melea, 31 Melea alikuwa mwana wa Mena, Mena alikuwa mwana wa Matatha, Matatha alikuwa mwana wa Nathani, Nathani alikuwa mwana wa Daudi, 32 Daudi alikuwa mwana wa Yese, Yese alikuwa mwana wa Obedi, Obedi alikuwa mwana wa Boazi, Boazi alikuwa mwana wa Salmoni, Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni, 33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu, Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu, Aramu alikuwa mwana wa Hesroni, Hesroni alikuwa mwana wa Peresi, Peresi alikuwa mwana wa Yuda, 34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo, Yakobo alikuwa mwana wa Isaki, Isaki alikuwa mwana wa Abrahamu, Abrahamu alikuwa mwana wa Tera, Tera alikuwa mwana wa Nahori, 35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi, Serugi alikuwa mwana wa Reu, Reu alikuwa mwana wa Pelegi, Pelegi alikuwa mwana wa Eberi, Eberi alikuwa mwana wa Sala, 36 Sala alikuwa mwana wa Kenani, Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi, Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu, Shemu alikuwa mwana wa Noa, Noa alikuwa mwana wa Lameki, 37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela, Methusela alikuwa mwana wa Enoki, Enoki alikuwa mwana wa Yaredi, Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli, Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani, 38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi, Enoshi alikuwa mwana wa Sethi, Sethi alikuwa mwana wa Adamu, Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

< Luka 3 >