< Luka 20 >

1 Siku moja, Yesu alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri habari njema, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, pamoja na wazee wa watu wakamjia. 2 Wakamuuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?” 3 Akawajibu, “Nami nitawauliza swali. 4 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” 5 Wakahojiana wao kwa wao wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 6 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yohana alikuwa nabii.” 7 Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.” 8 Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.” 9 Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. 11 Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza. 12 Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba. 13 “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’ 14 “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’ 15 Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.” “Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa? 16 Atakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa: “‘Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni’? 18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.” 19 Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu. 20 Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki ili wapate kumtega kwa maneno asemayo, ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala. 21 Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli. 22 Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” 23 Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia, 24 “Nionyesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni vya nani?” 25 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” 26 Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya. 27 Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza, 28 “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 29 Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto. 30 Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto, 31 naye wa tatu pia akamwoa. Vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke, na wote wakafa pasipo yeyote kupata mtoto. 32 Mwishowe, yule mwanamke naye akafa. 33 Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?” 34 Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. (aiōn g165) 35 Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi. (aiōn g165) 36 Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo. 37 Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Bwana, ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo.’ 38 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.” 39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umesema sawasawa kabisa!” 40 Baada ya hayo hakuna mtu aliyethubutu kumuuliza maswali tena. 41 Kisha Yesu akawaambia, “Imekuwaje basi wao husema Kristoni Mwana wa Daudi? 42 Daudi mwenyewe anasema katika Kitabu cha Zaburi: “‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, 43 hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.”’ 44 Ikiwa Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ basi atakuwaje mwanawe?” 45 Wakati watu wote walikuwa wanamsikiliza, Yesu akawaambia wanafunzi wake, 46 “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kukaa kwenye nafasi za heshima katika karamu. 47 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema, wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”

< Luka 20 >