< Yeremia 47 >

1 Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza: 2 Hili ndilo asemalo Bwana: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyomo ndani yake, miji na wale waishio ndani yake. Watu watapiga kelele; wote waishio katika nchi wataomboleza 3 kwa sauti ya kwato za farasi waendao mbio, kwa sauti ya magari ya adui na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea. 4 Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori. 5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe mpaka lini? 6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana, utaendelea mpaka lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’ 7 Lakini upanga utatuliaje wakati Bwana ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?”

< Yeremia 47 >