< Isaya 61 >

1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao; 2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi ya Mungu wetu, kuwafariji wote waombolezao, 3 na kuwapa mahitaji wale wanaohuzunika katika Sayuni, ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa. Nao wataitwa mialoni ya haki, pando la Bwana, ili kuonyesha utukufu wake. 4 Watajenga upya magofu ya zamani na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani; watafanya upya miji iliyoharibiwa, iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi. 5 Wageni watayachunga makundi yenu, wageni watafanya kazi katika mashamba yenu, na kutunza mashamba yenu ya mizabibu. 6 Nanyi mtaitwa makuhani wa Bwana, mtaitwa watumishi wa Mungu wetu. Mtakula utajiri wa mataifa, nanyi katika utajiri wao mtajisifu. 7 Badala ya aibu yao watu wangu watapokea sehemu maradufu, na badala ya fedheha watafurahia katika urithi wao; hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao, nayo furaha ya milele itakuwa yao. 8 “Kwa maana Mimi, Bwana, napenda haki, na ninachukia unyangʼanyi na uovu. Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao na kufanya agano la milele nao. 9 Wazao wao watajulikana miongoni mwa mataifa, na uzao wao miongoni mwa kabila za watu. Wale wote watakaowaona watatambua kuwa ni taifa ambalo Bwana amelibariki.” 10 Ninafurahia sana katika Bwana, nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu. Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu, na kunipamba kwa joho la haki, kama vile bwana arusi apambavyo kichwa chake kama kuhani, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vito vyake vya thamani. 11 Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota, na bustani isababishavyo mbegu kuota, ndivyo Bwana Mwenyezi atafanya haki na sifa zichipuke mbele ya mataifa yote.

< Isaya 61 >