< Isaya 56 >

1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Dumisheni haki na mkatende lile lililo sawa, kwa maana wokovu wangu u karibu na haki yangu itafunuliwa upesi. 2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili, mtu yule alishikaye kwa uthabiti, yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.” 3 Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme, “Hakika Bwana atanitenga na watu wake.” Usimwache towashi yeyote alalamike akisema, “Mimi ni mti mkavu tu.” 4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa matowashi washikao Sabato zangu, ambao huchagua kile kinachonipendeza na kulishika sana agano langu: 5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: nitawapa jina lidumulo milele, ambalo halitakatiliwa mbali. 6 Wageni wanaoambatana na Bwana ili kumtumikia, kulipenda jina la Bwana, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana agano langu: 7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.” 8 Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye Waisraeli waliohamishwa: “Bado nitawakusanya wengine kwao zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.” 9 Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni, njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni! 10 Walinzi wa Israeli ni vipofu, wote wamepungukiwa na maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kubweka; hulala na kuota ndoto, hupenda kulala. 11 Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. 12 Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo! Tunywe kileo sana! Kesho itakuwa kama leo, au hata bora zaidi.”

< Isaya 56 >