< Ezekieli 15 >

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora zaidi kuliko tawi la mti mwingine wowote ndani ya msitu? 3 Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza chochote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuningʼinizia vitu kutokana na huo mti wake? 4 Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lolote? 5 Kama haukufaa kitu chochote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa chochote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuunguza? 6 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati kwa ajili ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu waishio Yerusalemu. 7 Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nami nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kwamba Mimi ndimi Bwana. 8 Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema Bwana Mwenyezi.”

< Ezekieli 15 >