< Torati 22 >

1 Kama ukimwona ngʼombe au kondoo wa ndugu yako anapotea, usipuuze, bali uhakikishe unamrudisha kwa mwenyewe. 2 Ikiwa huyo ndugu haishi karibu nawe au kama hufahamu yeye ni nani, mchukue nyumbani kwako huyo mnyama umweke mpaka mwenyewe aje kumtafuta. Ndipo umrudishie. 3 Fanya vivyo hivyo ukimkuta punda wa nduguyo au joho lake au chochote alichopoteza. Usipuuze jambo hilo. 4 Kama ukimwona punda wa nduguyo au ngʼombe wake ameanguka barabarani, usipuuze jambo hilo. Msaidie asimame kwa miguu yake. 5 Haimpasi mwanamke kuvaa nguo za kiume wala mwanaume kuvaa nguo za kike, kwa maana Bwana Mungu wenu anachukia yeyote ambaye hufanya hivi. 6 Kama ukikuta kiota cha ndege kando ya barabara, iwe juu ya mti au chini, naye ndege amelala juu ya makinda au mayai, usimchukue huyo ndege pamoja na makinda yake. 7 Waweza kuchukua makinda, lakini uwe na hakika ya kumwacha huyo ndege, ili upate kufanikiwa na uweze kuishi maisha marefu. 8 Wakati unapojenga nyumba mpya, fanya ukuta wa kuzuia kandokando ya dari ili usijiletee hatia ya kumwaga damu juu ya nyumba yako ikiwa yeyote ataanguka kutoka humo. 9 Usipande aina mbili za mbegu katika shamba lako la mizabibu; ikiwa utafanya hivyo, si mazao utakayopanda tu yatakuwa najisi, bali nayo matunda ya shamba la mizabibu pia. 10 Usilime kwa maksai aliyefungwa nira pamoja na punda. 11 Usivae nguo za sufu na kitani zilizofumwa pamoja. 12 Fanya vishada kwenye pembe nne za joho unalovaa. 13 Ikiwa mtu atamwoa mke na, baada ya kufanya naye tendo la ndoa, akamchukia, 14 akimsingizia na kumwita jina baya, akisema, “Nilimwoa mwanamke huyu, lakini nilipomkaribia sikupata uthibitisho wa ubikira wake” 15 ndipo baba na mama wa msichana wataleta uthibitisho kwamba alikuwa bikira kwa wazee wa mji kwenye lango. 16 Baba wa msichana atawaambia wazee, “Nilimwoza binti yangu kwa huyu mwanaume, lakini hampendi. 17 Sasa amemsingizia na kusema, ‘Sikumkuta huyu binti akiwa bikira.’ Lakini hapa kuna uthibitisho wa ubikira wa binti yangu.” Kisha wazazi wake wataonyesha nguo zake kwa wazee wa mji, 18 nao wazee watamchukua huyo mwanaume na kumwadhibu. 19 Watamtoza shekeli mia moja za fedha na kupewa wazazi wa msichana, kwa sababu mwanaume huyu amempa bikira wa Kiisraeli jina baya. Ataendelea kuwa mke wake; kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake. 20 Hata hivyo, kama shtaka ni la kweli na hakuna uthibitisho juu ya ubikira wa huyo msichana ulioweza kupatikana, 21 huyo msichana ataletwa kwenye mlango wa nyumba ya baba yake, na hapo watu wa mji wake watampiga kwa mawe hadi afe. Amefanya kitu cha aibu katika Israeli kwa kufanya ukahaba akiwa nyumbani kwa babaye. Lazima mwondoe uovu katikati yenu. 22 Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli. 23 Ikiwa mwanaume atakutana na bikira mjini ambaye ameposwa na mtu akazini naye, 24 utawachukua wote wawili kwenye lango la mji na kuwapiga kwa mawe mpaka wafe; yule msichana kwa kuwa alikuwa mjini na hakupiga kelele kuomba msaada, na yule mwanaume kwa sababu amemtenda jeuri mke wa mtu mwingine. Lazima mwondoe uovu katikati yenu. 25 Lakini ikiwa itatokea mwanaume akakutana na msichana aliyeposwa huko mashambani, akambaka, mwanaume aliyefanya hivi peke yake ndiye atakayeuawa. 26 Usimtendee msichana yule jambo lolote; hajafanya dhambi inayostahili kifo. Shauri hili ni kama lile la yeyote ambaye anamshambulia na kumuua kwa makusudi jirani yake, 27 kwa maana mwanaume huyo alimkuta msichana huko mashambani, na ingawa msichana aliyeposwa alipiga kelele, hapakuwa na mtu wa kumwokoa. 28 Ikiwa itatokea mwanaume akutane na bikira ambaye hajaposwa na kumbaka nao wakakutwa, 29 mwanaume atamlipa baba wa msichana shekeli hamsini za fedha. Ni lazima amwoe huyo msichana, kwa maana amemfanyia jeuri. Kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake. 30 Mwanaume asimwoe mke wa baba yake; kamwe asidhalilishe kitanda cha baba yake.

< Torati 22 >