< Torati 15 >

1 Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2 Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. 3 Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4 Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5 ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. 6 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi. 7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu. 12 Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru. 13 Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu. 14 Mpe kwa uhuru kutoka zizi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka na kutoka mashinikizo yako ya kukamulia divai. Mpe kama vile ambavyo Bwana Mungu wako alivyokubariki. 15 Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Bwana Mungu wenu aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo. 16 Lakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe, 17 ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake mpaka hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mtumishi wa kike. 18 Usifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Bwana Mungu wenu atakubarikia kwa kila kitu utakachofanya. 19 Wekeni wakfu kwa Bwana Mungu wenu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ngʼombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo. 20 Kila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua. 21 Kama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Bwana Mungu wenu. 22 Itawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote wasio safi na walio safi kwa desturi za kiibada mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu. 23 Lakini kamwe msinywe damu; imwageni ardhini kama maji.

< Torati 15 >