< Danieli 11 >

1 Nami katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.) 2 “Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme watatu zaidi watatokea Uajemi, kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Wakati atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani. 3 Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, ambaye atatawala kwa nguvu nyingi na kufanya anavyopenda. 4 Baada ya kujitokeza, milki yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautakwenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizotumia, kwa sababu milki yake itangʼolewa na kupewa wengine. 5 “Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko mfalme, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi. 6 Baada ya miaka kadha, wataungana. Binti wa mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini huyo binti nguvu zake hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, watoto wake, na yeyote aliyemuunga mkono. 7 “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao naye atashinda. 8 Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadha atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua. 9 Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi nyuma hadi kwenye nchi yake. 10 Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini. 11 “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye ataunda jeshi kubwa, lakini litashindwa. 12 Wakati jeshi litakapokuwa limechukuliwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi na atachinja maelfu mengi, hata hivyo hatabaki na ushindi. 13 Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi jingine kubwa kuliko lile la kwanza; na baada ya miaka kadha, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri. 14 “Katika nyakati hizo wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio. 15 Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzunguka mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kuyazuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu ya kuwakabili. 16 Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza. 17 Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia. 18 Ndipo atabadili nia yake kupigana na nchi za pwani na ataziteka nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake na kurudisha ufidhuli wake juu yake. 19 Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. 20 “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita. 21 “Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona wako salama, naye atautwaa kwa hila. 22 Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake; jeshi pamoja na mkuu mmoja wa agano wataangamizwa. 23 Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, na akitumia watu wachache tu ataingia madarakani. 24 Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atafanikisha kile ambacho baba zake wala babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atafanya hila ya kupindua miji yenye maboma, lakini kwa muda mfupi tu. 25 “Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya kwa hila zilizofanywa dhidi yake. 26 Wale wanaokula kutoka kwenye ruzuku za mfalme watajaribu kumwangamiza; jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani. 27 Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya, wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamriwa. 28 Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume na agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano, kisha atarudi nchi yake. 29 “Wakati ulioamriwa, atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza. 30 Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atarudi nyuma na kutoa wazi hasira yake dhidi ya agano takatifu. Atarudi na kuonyesha fadhili kwa wale waliachao agano takatifu. 31 “Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu, na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu lisababishalo ukiwa. 32 Kwa udanganyifu atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti. 33 “Wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa au kufanywa mateka. 34 Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi ambao si waaminifu wataungana nao. 35 Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa mpaka wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamriwa. 36 “Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajasikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitokee. 37 Hataonyesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote. 38 Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani na zawadi za thamani kubwa. 39 Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala juu ya watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama. 40 “Katika wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko. 41 Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake. 42 Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka. 43 Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na utajiri wote wa Misri, pamoja na Walibia na Wakushi kwa kujisalimisha. 44 Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu kabisa wengi. 45 Atasimika hema zake za ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.

< Danieli 11 >