< 1 Samweli 22 >

1 Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
Basi Daudi aliondoka hapo na akatoroka kwenda kwenye pango la Adulamu. Kaka zake na wote wa nyumba ya baba yake waliposikia hayo, wakateremka kumwendea huko.
2 Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye.
Kila mmoja aliyekuwa na mahangaiko, kila mmoja aliyekuwa na deni, na kila mmoja ambaye hakuwa na furaha moyoni-wote walijikusanya kwake, na Daudi akawa jemedari wao. Kulikuwa na wanaume wapatao mia nne waliokuwa pamoja naye.
3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa huko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe mpaka nijue nini Mungu atakachonifanyia.”
Kisha Daudi alitoka huko akaenda Mispa huko Moabu. Akamwambia mfalme wa Moabu, “Tafadhali waruhusu baba na mama yangu wakae kwako hadi hapo nitakapojua kitu gani ambacho Mungu atafanya kwa ajili yangu.”
4 Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.
Basi akawaacha kwa Mfalme wa Moabu. Baba na mama yake wakakaa na mfalme kwa muda wote ambao Daudi alikuwa kwenye ngome yake.
5 Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi.
Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae tena katika ngome yako. Ondoka na uende katika nchi ya Yuda.” Kwa hiyo Daudi akatoka hapo na akaenda katika msitu wa Harethi.
6 Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka.
Sauli akasikia kwamba Daudi amepatikana, akiwa pamoja na watu aliokuwa nao. Wakati huo Sauli alikuwa akikaa Gibea chini ya mti wa mkwaju huko Rama, akiwa na mkuki wake mkononi mwake, na watumishi wake wote walikuwa wamesimama wamemzunguka.
7 Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi watu wa Benyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia?
Sauli akawaambia watumishi wake, Sasa sikilizeni, watu wa Benyamini! Je, mwana wa Yese atawapa mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya nyote kuwa majemedari wa maelfu na majemedari wa mamia,
8 Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.”
hata ninyi nyote mnapanga njama dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu anayenijulisha kwamba mwanangu anafanya agano na mwana wa Yese. Hakuna hata mmoja wenu anayenionea huruma. Hakuna hata mmoja wenu anayenijulisha kwamba mwanangu anamchochea mtumishi wangu Daudi awe kinyume changu. Leo mejificha na ananisubiri ili anishambulie.”
9 Lakini Doegi Mwedomu, ambaye alikuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu.
Kisha Doegi Mwedomu, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akajibu, Nilimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu.
10 Ahimeleki akamuuliza Bwana kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.”
Alimwomba BWANA ili apate kumsaidia, na alimpatia mahitaji na upanga wa Goliathi, Mfilisti”
11 Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme.
Kisha Mfalme akamtuma mtu amwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu na watu wote wa nyumba ya baba yake, makuhani waliokuwa huko Nobu. Wote walifika mbele ya mfalme.
12 Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.” Akajibu, “Naam, bwana wangu.”
Sauli akasema, “Sasa sikiliza, mwana wa Ahitubu,” Naye akajibu, “Niko hapa, bwana wangu.”
13 Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga shauri baya dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena hukumuuliza Mungu kwa ajili yake, na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?”
Sauli akamwambia, “Kwa nini unapanga njama dhidi yangu, wewe pamoja na mwana wa Yese, kwa kumpatia mikate, na upanga, na umemwomba Mungu kusudi amsaidie Daudi, kusudi aniasi mimi, na kujificha sehemu ya siri, kama alivyofanya leo?”
14 Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako?
Ndipo Ahimeleki akamjibu mfalme na kusema, “Je, ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliyemwaminifu kama Daudi, ni nani mkwe wa mfalme na yuko juu ya walinzi wako, na mwenye heshima nyumbani mwako?
15 Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.”
Je, leo ni mara ya kwanza kwangu kumuomba Mungu apate kumsaidia? Hapana! Mfalme usinilaumu mimi mtumishi wako kwa jambo lolote wala jamaa zangu wote. Maana mimi mtumishi wako sijui lolote kuhusu kadhia hii.”
16 Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
Mfalme akamjibu, “Hakika utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya nyumba ya baba yako.”
17 Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Bwana, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.” Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Bwana.
Mfalme akamwambia mlinzi aliyesimama karibu naye, “Geuka na uwauwe makuhani wa BWANA. Kwa sababu wanamuunga mkono Daudi, na sababu walijua kwamba alikimbia, lakini hawakunijulisha.” Lakini watumishi wa mfalme hawakunyoosha mkono wao kuwaua makuhani wa BWANA.
18 Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano wavaao visibau vya kitani.
Ndipo mfalme akamwambia Doegi, “Geuka na uwauwe makuhani.” Hivyo Doegi Mwedomu akageuka na kuwapiga makuhani; akawaua watu themanini na watano waliovaa naivera ya kitani siku hiyo.
19 Pia akaupiga Nobu kwa upanga, mji wa makuhani, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto wadogo na wale wanyonyao, ngʼombe wake, punda na kondoo.
Kwa ncha ya upanga, aliupiga Nobu, mji wa makuhani, akiwaua wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ng'ombe na punda na kondoo. Wote aliwaua kwa ncha ya upanga.
20 Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi.
Lakini mmoja wa wana wa Ahimeleki mwana wa Ahitubu, aliyeitwa Abiathari, aliponyoka na kukimbilia kwa Daudi.
21 Akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Bwana.
Abiathari akamwambia Daudi kwamba Sauli amewaua manabii wa BWANA.
22 Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile, wakati Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli. Mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa ya baba yako yote.
Daudi akamwambia Abiathari, “Nilifahamu kuwa siku hiyo, Doegi Mwedomu alikuwa mahali pale, kwamba hakika angemwambia Sauli. Nina wajibika kwa kifo cha kila mtu katika familia ya baba yako!
23 Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”
Kaa pamoja nami na usiogope. Maana mtu anayetafuta roho yako anatafuta pia roho yangu. Utakuwa salama ukiwa pamoja nami.”

< 1 Samweli 22 >