< Marko 2 >

1 Aliporudi Kaperinaumu baada ya siku chache, ilisikika kwamba alikuwa nyumbani. 2 Watu wengi sana walikuwa wamekusanyika pale na haikuwepo nafasi tena, hata ile ya pale mlangoni, na Yesu alisema neno kwao. 3 Kisha baadhi ya watu walikuja kwake waliomleta mtu aliyekuwa amepooza; watu wanne walikuwa wamembeba. 4 Wakati waliposhindwa kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu, waliondoa paa juu ya mahali pale alipokuwa. Na walipokuwa wamekwishatoboa tundu, walishusha kitanda ambacho mtu aliyepooza alikuwa amelala. 5 Alipoiona imani yao, Yesu alimwambia mtu aliyepooza, “mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.” 6 Lakini baadhi ya waandishi wale waliokuwa wamekaa pale walijihoji mioyoni mwao, 7 “Anawezaje mtu huyu kusema hivi? Anakufuru! Nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” 8 Mara Yesu alijua rohoni mwake walichokuwa wakifikiri miongoni mwao wenyewe. Aliwaambia, “Kwa nini mnafikiri hivi mioyoni mwenu? 9 Lipi ni jepesi zaidi kusema kwa mtu aliyepooza, 'Dhambi zako zimesamehewa' au kusema 'Simama, chukua kitanda chako, na utembee?' 10 Lakini ili wapate kujua ya kuwa Mwana wa Adamu ana mamlaka ya kusamehe dhambi katika dunia, alimwambia yule aliyepooza, 11 “Nakuambia wewe, inuka, chukua mkeka wako, na uende nyumbani kwako.” 12 Alisimama na mara moja akachukua mkeka wake, na alikwenda nje ya nyumba mbele ya kila mtu, hivyo wote walishangaa na walimpa Mungu utukufu, na wakasema “Kamwe, hatujawahi kuona jambo kama hili.” 13 Alienda tena kando ya ziwa, na umati wote wa watu walikuja kwake, na akawafundisha. 14 Alipokuwa akipita alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi kwenye sehemu ya kukusanyia kodi na akamwambia, “Nifuate.” Alisimama na kumfuata. 15 Na wakati Yesu alipokuwa akipata chakula katika nyumba ya Lawi, wakusanya kodi wengi na watu wenye dhambi walikuwa wakila na Yesu na wanafunzi wake, kwa kuwa walikuwa wengi nao walimfuata. 16 Wakati waandishi, ambao walikuwa Mafarisayo, walipoona kwamba Yesu alikuwa akila na watu wenye dhambi na wakusanya kodi, waliwaambia wanafunzi wake, “Kwa nini anakula na wakusanya kodi na watu wenye dhambi?” 17 Wakati Yesu aliposikia hivi aliwaambia, “Watu walio na afya katika mwili hawamhitaji tabibu; ni watu wagonjwa pekee ndio wanamhitaji. Sikuja kuwaita watu wenye haki, lakini watu wenye dhambi.” 18 Wanafunzi wa Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Na baadhi ya watu walikuja kwake na kumwambia, “Kwa nini wanafunzi wa Yohana na mafarisayo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi? 19 Yesu aliwaambia, “Je waliohudhuria harusini wanaweza kufunga wakati bwana harusi bado akiwa pamoja nao? Kwa vyovyote bwana harusi akiwa bado yuko pamoja nao hawawezi kufunga.” 20 Lakini siku zitakuja wakati bwana harusi atakapoondolewa kwao, na katika siku hizo wao watafunga. 21 Hakuna mtu ashonaye kipande kipya cha nguo kwenye vazi kuukuu, vinginevyo kiraka kitabanduka kutoka katika hilo, kipya kubanduka kutoka katika kikuukuu, na kutakuwepo mpasuko mbaya. 22 Hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu, vinginevyo divai itavipasua viriba na vyote viwili divai na viriba vitapotea. Badala yake, weka divai mpya katika viriba vipya.” 23 Katika siku ya Sabato Yesu alipita kwenye baadhi ya mashamba, na wanafunzi wake walianza kuchukua baadhi ya masuke ya ngano. 24 Na Mafarisayo walimwambia, “Tazama, kwa nini wanafanya kitu ambacho ni kinyume cha sheria katika siku ya Sabato?” 25 Aliwaambia, “Hamkusoma kile alichofanya Daudi alipokuwa katika uhitaji na njaa—yeye pamoja na watu waliokuwa pamoja naye? 26 Jinsi alivyoenda katika nyumba ya Mungu wakati Abiathari alipokuwa kuhani mkuu na akala mkate uliowekwa mbele—ambao ilikuwa kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kula isipokuwa makuhani—na aliwapa hata baadhi ya wale waliokuwa pamoja naye?” 27 Yesu alisema, “Sabato ilifanywa kwa ajili ya mwanadamu, siyo mwanadamu kwa ajili ya Sabato. 28 Kwa hiyo, Mwana wa Adamu ni Bwana, hata kwa Sabato.”

< Marko 2 >