< Yuda 1 >

1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, na ndugu yake Yakobo, kwa wale ambao wameitwa, wapendwao katika Mungu Baba, na waliotunzwa kwa ajili ya Yesu Kristo:
Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo.
2 rehema na amani na upendo viongezwe kwenu.
Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
3 Wapenzi, wakati nilipokuwa nikifanya kila juhudi kuwaandikia ninyi kuhusu wokovu wetu sote, ilinilazimu kuwaandikia kwa ajili ya kuwashauri ili mshindanie kwa uaminifu imani ambayo ilikuwa imekabidhiwa mara moja tu kwa waamini.
Ndugu wapenzi, wakati nimo katika jitihada ya kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, nimeona lazima ya kuwaandikieni na kuwahimizeni mwendelee kupigana kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote.
4 Kwa sababu watu fulani wamejiingiza kwa siri kati yenu - watu ambao walitiwa alama kwa ajili ya hukumu - watu wasio wataua ambao hubadili neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, na kumkana Bwana wetu pekee na Bwana Yesu Kristo.
Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake kiongozi na Bwana wetu. Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu awali hukumu inayowangojea watu hao.
5 Sasa napenda kuwakumbusha ninyi ingawa kuna wakati mlijua kwa ukamilifu kwamba Bwana aliwaokoa watu kutoka nchi ya Misri, lakini baadaye kuwaangamiza wale ambao hawakuamini.
Nataka kuwakumbusheni mambo fulani ambayo mmekwisha yajua: kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
6 Na malaika ambao hawakuilinda enzi yao wenyewe lakini wakaacha makao yao maalum Mungu amewaweka katika minyororo ya milele, ndani ya giza, kwa ajili ya hukumu ya siku ile kuu. (aïdios g126)
Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe Siku ile kuu. (aïdios g126)
7 Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyoizunguka, ambayo pia ilijiingiza yenyewe katika uasherati na wakafuata tamaa isiyo ya asili. Walioneshwa kama mifano ya wale ambao huteseka katika hukumu ya moto wa milele. (aiōnios g166)
Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. (aiōnios g166)
8 Hali kadhalika, kwa njia ile ile waota ndoto hawa pia huchafua miili yao, na hukataa mamlaka, na wananena uongo dhidi ya mtukufu.
Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu.
9 Lakini hata Mikaeli malaika mkuu, wakati alipokuwa akishindana na ibilisi na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kuleta hukumu ya uongo dhidi yake, lakini badala yake alisema, “Bwana akukemee!”
Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi waliobishana juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi; ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.”
10 Lakini watu hawa huleta uongo dhidi ya chochote wasicho kifahamu. Na kile wasicho kifahamu- kile ambacho wanyama wasio na akili hujua kwa silika- haya ndiyo yaliyo waharibu.
Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama vile wanyama wanayoyajua ndiyo yanayowaangamiza.
11 Ole wao! Kwa kuwa wametembea katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu. Wameangamia katika uasi wa Kora.
Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Baalamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa.
12 Hawa ni miamba katika sherehe zenu za upendo, wakisherehekea bila aibu, wakijilisha tu wenyewe. Ni mawingu yasiyo na maji, yanayobebwa na upepo, ni miti iliyopukutika isiyo na matunda iliyo kufa mara mbili, iliyong'olewa mizizi
Kwa makelele yao yasiyo na adabu, watu hao ni kama madoa machafu katika mikutano yenu ya karamu ya Bwana. Hujipendelea wao wenyewe tu, na wako kama mawingu yanayopeperushwa huko na huko na upepo bila ya kuleta mvua. Wao ni kama miti isiyozaa matunda hata wakati wa majira yake, wamekufa kabisa.
13 Ni mawimbi ya bahari yenye kelele yakitoa aibu yao wenyewe, Ni nyota zinazorandaranda ambazo weusi wa giza umetunzwa kwa ajili yao milele. (aiōn g165)
Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanaonekana dhahiri kama vile mapovu ya mawimbi. Wao ni kama nyota zinazotangatanga, ambao Mungu amewawekea mahali pao milele katika giza kuu. (aiōn g165)
14 Enoko, wa saba katika orodha ya Adamu, alitabiri kuhusu wao, akisema, “Tazama! Bwana anakuja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake,
Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hawa: “Sikilizeni! Bwana atakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu
15 ili afanye hukumu juu ya kila mtu, na kutia hatia wote wasiomcha Mungu juu ya matendo yao yote waliyokwishafanya katika njia zisizo za kitauwa, na kwa maneno yote ya ukali ambayo wasio watauwa wameyanena dhidi yake.”
kutoa hukumu juu ya binadamu wote, kuwahukumu wote kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16 Hawa ni wale wanung'unikao, walalamikao ambao hufuata tamaa zao za uovu, wajivunao mno, ambao kwa faida yao hudanganya wengine.
Watu hawa wananung'unika daima na kuwalaumu watu wengine. Hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kusudi wafaulu katika mipango yao.
17 Lakini ninyi, wapenzi, kumbukeni maneno ambayo yalinenwa zamani na mitume wa Bwana Yesu Kristo.
Lakini ninyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali ni mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo.
18 Walisema kwenu, “Katika wakati wa mwisho kutakuwa na watu wanaodhihaki ambao hufuata tamaa zao zisizo za kitauwa.”
Waliwaambieni: “Siku za mwisho zitakapofika, watatokea watu watakaowadhihaki ninyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.”
19 Watu hawa ni watenganishaji, wanatawaliwa na tamaa za asili, na hawana Roho.
Hao ndio watu wanaosababisha mafarakano, watu wanaotawaliwa na tamaa zao za kidunia, watu wasio na Roho wa Mungu.
20 Lakini ninyi, wapenzi, kama mjijengavyo katika imani yenu takatifu sana, na kama muombavyo katika Roho Mtakatifu,
Lakini ninyi, wapenzi wangu, endeleeni kujijenga kikamilifu katika imani yenu takatifu. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,
21 jitunzeni katika upendo wa Mungu, na msubiri rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ambayo huwapatia uzima wa milele. (aiōnios g166)
na kubaki katika upendo wa Mungu, mkiwa mnamngojea Bwana wetu Yesu Kristo awapeni uzima wa milele kwa huruma yake. (aiōnios g166)
22 Onesheni rehema kwa wale walio na shaka.
Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka;
23 Waokoeni wengine kwa kuwanyakua kutoka katika moto. Kwa wengine onesheni huruma kwa hofu, mkichukia hata vazi lililotiwa doa na mwili.
waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni; na kwa wengine muwe na huruma pamoja na hofu, lakini chukieni hata mavazi yao ambayo yamechafuliwa na tamaa zao mbaya.
24 Sasa kwake awezaye kuwalinda msijikwae, na kuwasababisha msimame mbele ya utukufu wake, bila mawaa na kuwa na furaha kuu,
Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta ninyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake,
25 kwake Mungu pekee mwokozi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu uwe kwake, ukuu, uwezo na nguvu kabla ya nyakati zote, na sasa na hata milele. Amina. (aiōn g165)
kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina. (aiōn g165)

< Yuda 1 >