< Yohana 12 >

1 Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alienda Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye alimfufua kutoka katika wafu. 2 Basi wakamwandalia chakula cha jioni huko, na Martha akamtumikia, wakati huo Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu. 3 Kisha Mariamu akachukua ratli ya manukato yaliyotengenezwa kwa nardo safi, yenye thamani kubwa, akampaka Yesu miguuni, na kumfuta miguu kwa nywele zake; nyumba yote ilijaa harufu ya manukato. 4 Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi wake, ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, 5 “Kwanini manukato haya yasingeuzwa kwa dinari mia tatu na wakapewa maskini?” 6 Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini, bali kwa sababu alikuwa mwizi: yeye ndiye aliyeshika mfuko wa fedha na alikuwa anachukua baadhi ya vilivyowekwa humo kwa ajili yake mwenyewe. 7 Yesu alisema, “Mwache aweke alicho nacho kwa ajili ya siku ya maziko yangu. 8 Maskini mtakuwa nao siku zote; lakini hamtakuwa nami siku zote.” 9 Basi umati mkubwa wa Wayahudi walipata kujua ya kuwa Yesu yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili ya Yesu tu, ila wamwone na Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka katika wafu. 10 Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri ili wamue Lazaro; 11 maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walienda zao na wakamwamini Yesu. 12 Na siku ya pili yake umati mkubwa walikuja kwenye sikukuu. Waliposikia ya kuwa Yesu anakuja Yerusalemu, 13 walichukua matawi ya miti ya mitende na kutoka nje kwenda kumlaki na wakapiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli.” 14 Yesu alimpata mwana-punda akampanda; kama vile ilivyoandikwa, 15 “Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.” 16 Wanafunzi wake hawakuyaelewa mambo haya hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kuwa mambo haya aliandikiwa yeye na ya kwamba wametenda mambo haya kwake. 17 Basi lile kundi la watu waliokuwepo pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, wakashuhudia kwa wengine. 18 Na ilikuwa kwa sababu hii pia kwamba kundi la watu walikwenda kumlaki kwasababu walisikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo. 19 Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, “Tazama, sasa hamwezi kufanya lolote; tazama, ulimwengu umekwenda kwake.” 20 Sasa baadhi ya Wayunani walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakienda kuabudu kwenye sikukuu. 21 Hawa walimwendea Filipo, ambaye alitoka Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba wakisema, “Bwana, sisi tunatamani kumwona Yesu.” 22 Filipo akaenda akamwambia Andrea; Andrea na Filipo wakaenda na kumwambia Yesu. 23 Yesu akawajibu akasema, “Saa imefika kwa ajili ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24 Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, itazaa matunda mengi. 25 Yeye apendaye uhai wake ataupoteza; bali yeye auchukiaye uhai wake katika ulimemngu huu atausalimisha hata uzima wa milele. (aiōnios g166) 26 Mtu yeyote akinitumikia mimi, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Mtu yeyote akinitumikia, Baba atamheshimu. 27 Sasa roho yangu imefadhaika: nami nisemeje? 'Baba, uniokoe katika saa hii'? Lakini ni kwa kusudi hii nimeifikia saa hii. 28 Baba, ulitukuze jina lako.” Kisha sauti ikaja kutoka mbinguni na kusema, “Nimelitukuza nami nitalitukuza tena.” 29 Basi mkutano uliosimama karibu naye wakasikia, wakasema ya kwamba kumekuwa ngurumo. Wengine walisema, “Malaika amesema naye.” 30 Yesu akajibu na kusema, “Sauti hii haikuja kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. 31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo: Sasa mkuu wa ulimwngu huu atatupwa nje. 32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.” 33 Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa. 34 Mkutano wakamjibu, “Sisi tumesikia katika sheria ya kwamba Kristo atadumu hata milele. Nawe wasemaje, 'Mwana Adamu lazima ainuliwe juu'? Huyu Mwana wa Mtu ni nani?” (aiōn g165) 35 Basi Yesu akawaambia, “Nuru ingalipo pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru, ili kwamba giza lisije likawaweza. Yeye aendaye gizani hajui aendako. 36 Mngali mnayo nuru, iaminini nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Yesu aliyasema haya na kisha akaenda zake akajificha wasimwone. 37 Ingawa Yesu alifanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, bado hawakumwamini 38 ili litimie neno la nabii Isaya, alilosema: “Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?” 39 Ndio sababu wao hawakuamini, maana Isaya alisema tena, 40 “Amewapofusha macho, na ameifanya migumu mioyo yao; wasije wakaona kwa macho yao na wakafahamu kwa mioyo yao, na wakaongoka nami nikawaponya.” 41 Isaya alisema maneno hayo kwa kuwa aliuona utukufu wa Yesu na akanena habari zake. 42 Walakini, hata wakuu wengi walimwamini Yesu; lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakukiri ili wasije wakatengwa na sinagogi. 43 Walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu. 44 Yesu akapaza sauti na kusema, “Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi tu bali na yeye aliyenituma mimi, 45 naye anionaye mimi anamuona yeye aliyenituma. 46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. 47 Ikiwa mtu yeyote atayasikia maneno yangu lakini asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, bali niuokoe ulimwengu. 48 Yeye anikataye mimi na asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye: neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. 49 Maana mimi sikunena kwa nafsi yangu tu. Bali ni Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. 50 Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi - kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo kwao.” (aiōnios g166)

< Yohana 12 >