< Wahebrania 6 >

1 Kwa hiyo, tukiacha tulichojifunza kwanza kuhusu ujumbe wa Kristo, twapaswa kuwa na juhudi kuelekea kwenye ukomavu, tusiweke tena misingi ya toba kutoka katika kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2 wala misingi ya mafundisho ya ubatizo, na kuwawekea mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. (aiōnios g166) 3 Na tutafanya hivi ikiwa Mungu ataruhusu. 4 Kwa kuwa haiwezekani kwa wale ambao waliipata nuru awali, ambao walionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa kuwa washirika wa Roho Mtakatifu, 5 na ambao walionja uzuri wa neno la Mungu na kwa nguvu za wakati ujao, (aiōn g165) 6 na kisha wakaanguka - haiwezekani kuwarejesha tena katika toba. Hii ni kwa sababu wamemsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, wakimfanya kuwa chombo cha dhihaka hadharani. 7 Kwa kuwa ardhi iliyopokea mvua inyeshayo mara kwa mara juu yake, na ikatoa mazao muhimu kwa hao waliofanya kazi katika ardhi, hupokea baraka kutoka kwa Mungu. 8 Lakini ikiwa huzaa miiba na magugu, haina tena thamani na ipo katika hatari ya kulaaniwa. Mwisho wake ni kuteketezwa. 9 Ijapokuwa tunazungumza hivi, rafiki wapenzi, tunashawishiwa na mambo mazuri yawahusuyo ninyi na mambo yahusuyo wokovu. 10 Kwa kuwa Mungu si dhalimu hata asahau kazi yenu na kwa upendo mliouonesha kwa ajili ya jina lake, katika hili mliwatumikia waamini na bado mngali mnawatumikia. 11 Na tunatamani sana kwamba kila mmoja wenu aweze kuonesha bidii ile ile mpaka mwisho kwa uhakika wa ujasiri. 12 Hatutaki muwe wavivu, lakini muwe wafuasi wa wale warithio ahadi kwa sababu ya imani na uvumilivu. 13 Kwa maana Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa nafsi yake, kwa kuwa asingeliapa kwa mwingine yeyote aliye mkubwa kuliko yeye. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki, na nitauongeza uzao wako zaidi.” 15 Kwa njia hii, Abrahamu alipokea kile alichoahidiwa baada ya kusubiria kwa uvumilivu. 16 Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, na kwao ukomo wa mashindano yote ni kiapo kwa kuyathibitisha. 17 Wakati Mungu alipoamua kuonesha kwa uwazi zaidi kwa warithi wa ahadi kusudi lake zuri lisilobadilika, alilithibitisha kwa kiapo. 18 Alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi tulioikimbilia hifadhi tupate kutiwa moyo kushikilia kwa nguvu tumaini lililowekwa mbele yetu. 19 Tunao ujasiri huu kama nanga imara na ya kutegemea ya roho zetu, ujasiri ambao unaingia sehemu ya ndani nyuma ya pazia. 20 Yesu aliingia sehemu ile kama mtangulizi wetu, akisha kufanyika kuhani mkuu hata milele baada ya utaratibu wa Melkizedeki. (aiōn g165)

< Wahebrania 6 >