< Mwanzo 4 >

1 Mwanume akalala na Hawa mke wake. Akabeba mimba na akamzaa Kaini. Akasema, “nimezaa mwanaume kwa msaada wa Yahwe.” 2 Kisha akazaa ndugu yake Habili. Sasa Habili akawa mchungaji, lakini Kaini alilima udongo. 3 Ikawa kwamba baada ya muda Kaini alileta sehemu ya mazao ya ardhi kama sadaka kwa Yahwe. 4 Habili pia, alileta sehemu ya wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona. Yahwe akamkubali Habili pamoja na sadaka yake, 5 lakini Kaini pamoja na sadaka yake Mungu hakuikubali. Kwa hiyo Kaini alikasirika sana, na uso wake ukakunjamana. 6 Yahwe akamwambia Kaini, “kwa nini umekasirika na kwa nini uso wako umekunjamana? 7 Kama ukifanya vema, je hutapata kibali? lakini kama hutafanya lilio jema, dhambi iko inakuotea mlangoni na inatamani kukutawala, lakini inakupasa uishinde. 8 Kaini akamwambia Habili ndugu yake. Hata wakati walipokuwa shambani, Kaini aliinuka dhidi ya Habili ndugu yake na akamuua. (Katika tafsiri za kale zinasema, Kaini alimwambia Habili ndugu yake, “twende mashambani.” Na wakati walipokuwa shambani, Kaini alimuinukia Habili ndugu yake na kumuua). 9 Kisha Yahwe akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akasema, “sijui. Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” 10 Yahwe akasema, “umefanya nini? damu ya ndugu yako inaniita mimi kutokea ardhini. 11 Na sasa umelaaniwa wewe kutoka ardhi ambayo imefungua kinywa chake kupokea damu ya ndugu yako kutoka mikononi mwako. 12 Utakapo ilima ardhi, kuanzia sasa na kuendelea haita kuzalia wewe nguvu yake. Utakuwa mkimbizi na mtu asiye na makao duniani.” 13 Kaini akamwambia Yahwe, “Adhabu yangu ni kubwa kuliko uwezo wangu wa kustahimili. 14 Kwa hakika umenifukuza siku hii ya leo kutoka kwenye ardhi hii, na sitaonekana mbele ya uso wako. Nitakuwa mkimbizi na mtu nisiye na makao katika dunia, na yeyote atakaye niona ataniua.” 15 Yahwe akamwambia, “ikiwa mtuyeyote atamuua Kaini, kisasi kitakuwa juu yake mara saba.” Kisha Yahwe akaweka alama juu ya Kaini, ili kwamba kama mtu awayeyote akimuona, mtu huyo asimshambulie. 16 Kwa hiyo Kaini akatoka mbele ya uwepo wa Yahwe na akaishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni. 17 Kaini akamjua mke wake na akapata mimba. Akamzaa Henoko. Akajenga mji na akauita kwa jina la mwanae Henoko. 18 Kwa Henoko akazaliwa Iradi. Iradi akamzaa Mehuyaeli. Mehuyaeli akamzaa Methushaeli. Methushaeli akamzaa Lameki. 19 Lameki akajitwalia wake wawili: jinala mmoja alikuwa Ada, na jina la yule mwingine alikuwa Sila. 20 Ada akamzaa Yabali. Huyu ndiye alikuwa baba yao na wale walioishi hemani ambao wanafuga wanyama. 21 Ndugu yake aliitwa Yubali. Huyu alikuwa baba yao na wale wapigao kinubi na filimbi. 22 Sila naye akamzaa Tubal Kaini, mfua vyombo vya shaba na chuma. Dada yake na Tubal Kaini alikuwa Naama. 23 Lameki akawaambia wake zake, Ada na Sila, sikieni sauti yangu; ninyi wake wa Lameki, sikilizeni nisemacho. Kwa kuwa nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana kwa kunichubua. 24 Ikiwa Kaini atalipiwa kisasi mara saba, ndipo Lameki atalipiwa kisasi mara sabini na saba.” 25 Adam akamjua mke wake tena, na akazaa mtoto mwanaume. Akamuita jina lake Sethi na akasema, “Mungu amenipatia mtoto mwingine wa kiume kwa nafasi ya Habili, kwa kuwa Kaini alimuuwa.” 26 Mtoto wa kiume alizaliwa kwa Sethi na akamuita jina lake Enoshi. Wakati huo watu walianza kuliitia jina la Yahwe.

< Mwanzo 4 >