< Zekaria 13 >

1 “Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi. 2 “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. 3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo. 4 “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. 5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’ 6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’ 7 “Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu, dhidi ya mtu aliye karibu nami!” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika, nami nitageuza mkono wangu dhidi ya walio wadogo, 8 katika nchi yote,” asema Bwana, “theluthi mbili watapigwa na kuangamia; hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake. 9 Hii theluthi moja nitaileta katika moto; nitawasafisha kama fedha isafishwavyo na kuwajaribu kama dhahabu. Wataliitia Jina langu nami nitawajibu; nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’ nao watasema, ‘Bwana ni Mungu wetu.’”

< Zekaria 13 >