< Zaburi 84 >

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora. Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, makao yako yapendeza kama nini! 2 Nafsi yangu inatamani sana, naam, hata kuona shauku, kwa ajili ya nyua za Bwana; moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu Aliye Hai. 3 Hata shomoro amejipatia makao, mbayuwayu amejipatia kiota mahali awezapo kuweka makinda yake: mahali karibu na madhabahu yako, Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mfalme wangu na Mungu wangu. 4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wanaokusifu wewe daima. 5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako, na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao. 6 Wanapopita katika Bonde la Baka, hulifanya mahali pa chemchemi, pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi. 7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu, hadi kila mmoja afikapo mbele za Mungu huko Sayuni. 8 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu; nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo. 9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu, mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako. 10 Siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu kuliko kukaa katika mahema ya waovu. 11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao, Bwana hutoa wema na heshima; hakuna kitu chema anachowanyima wale ambao hawana hatia. 12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.

< Zaburi 84 >