< Zaburi 75 >

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Zaburi ya Asafu. Wimbo. Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu. 2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki. 3 Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara. 4 Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu. 5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’” 6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu. 7 Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine. 8 Mkononi mwa Bwana kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa mpaka tone la mwisho. 9 Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo. 10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.

< Zaburi 75 >