< Zaburi 65 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa. 2 Ewe usikiaye maombi, kwako wewe watu wote watakuja. 3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu. 4 Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu. 5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana, 6 uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu, 7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa. 8 Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha. 9 Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru. 10 Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake. 11 Umeuvika mwaka taji ya baraka, magari yako yanafurika kwa wingi. 12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha. 13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.

< Zaburi 65 >