< Zaburi 6 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 2 Unirehemu Bwana, kwa maana nimedhoofika; Ee Bwana, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali. 3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini? 4 Geuka Ee Bwana, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako. 5 Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa kuzimu? (Sheol h7585) 6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha nafurikisha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha viti vyangu vya fahari kwa machozi. 7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote. 8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu. 9 Bwana amesikia kilio changu kwa huruma, Bwana amekubali sala yangu. 10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.

< Zaburi 6 >