< Zaburi 4 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi. Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu. 2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu mpaka lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo mpaka lini? 3 Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; Bwana atanisikia nimwitapo. 4 Katika hasira yako, usitende dhambi. Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya mkiichunguza mioyo yenu. 5 Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni Bwana. 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonyesha jema lolote?” Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako. 7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi. 8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana, waniwezesha kukaa kwa salama.

< Zaburi 4 >