< Zaburi 24 >

1 Zaburi ya Daudi. Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake, ulimwengu, na wote waishio ndani yake, 2 maana aliiwekea misingi yake baharini na kuifanya imara juu ya maji. 3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana? Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake? 4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe, yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake au kuapa kwa kitu cha uongo. 5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Bwana, na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake. 6 Hiki ndicho kizazi cha wale wamtafutao, wale wautafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. 7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, inukeni enyi milango ya kale, ili mfalme wa utukufu apate kuingia. 8 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Ni Bwana aliye na nguvu na uweza, ni Bwana aliye hodari katika vita. 9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, viinueni juu enyi milango ya kale, ili Mfalme wa utukufu apate kuingia. 10 Ni nani yeye, huyu Mfalme wa utukufu? Ni Bwana Mwenye Nguvu Zote; yeye ndiye Mfalme wa utukufu.

< Zaburi 24 >