< Zaburi 18 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana aliyomwimbia Bwana wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi: Nakupenda wewe, Ee Bwana, nguvu yangu.
Nakupenda, Yahwe, nguvu yangu.
2 Bwana ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba, ambaye kwake ninakimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu.
Yahwe ni mwamba wangu, ngome yangu, yeye ambaye aniwekae kweye usalama; yeye ni Mungu wangu, mwamba wangu; ninapata kimbilio kwake. Yeye ni ngao yangu, pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
3 Ninamwita Bwana anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
Nitamuita Yahwe kwa sababu anastahili kusifiwa, na nitaokolewa kutoka kwa adui zangu.
4 Kamba za mauti zilinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
Kamba za mauti zilinizunguka, na mafuriko yakimbiayo yalinielemea.
5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. (Sheol h7585)
Kamba za kuzimu zilinizunguka; mitego ya mauti ilininasa. (Sheol h7585)
6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake.
dhiki yangu nilimuita Yahwe; Niliita msaada kwa Mungu. Naye alisikia sauti yangu kutoka hekaluni mwake; kuita kwangu msaada kulienda mpaka uweponi mwake; na kuingia masikioni pake.
7 Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
Kisha nchi ikatikisika na kutetemeka; misingi ya milima pia ilitetemeka na kutikiswa kwa sababu Mungu alikuwa amekasirika.
8 Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake.
Moshi ulifuka kutoka kwenye pua zake, na moto mkali ulitokea mdomoni mwake. Makaa yaliwashwa kwa moto huo.
9 Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
Yeye alizifunua mbingu na alishuka chini, na giza nene lilikuwa chini ya miguu yake.
10 Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mbawa za upepo.
Alipanda kwenye kerubi na akaruka; alinyiririka kwenye mabawa ya upepo.
11 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka, mawingu meusi ya mvua ya angani.
Yahwe alilifanya giza kuwa hema likimzunguka yeye, wingu la mvua zito katika mbingu.
12 Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikanyesha mvua ya mawe na umeme wa radi.
Mawe ya barafu na makaa ya moto yalianguka kutoka katika mwangaza kabla yake.
13 Bwana alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
Yahwe aliongea katika mbingu! Sauti ya aliye juu ilisikika.
14 Aliipiga mishale yake na kutawanya adui, naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
Yeye aliifyatua mishale yake na kuwatawanya adui zake; na radi nyingi zenye mwanga alizitawanya katika maeneo tofauti tofauti.
15 Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee Bwana, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
Ndipo mifereji ya maji ilitokea; misingi ya dunia ikadhihirishwa kwa mlio wa pigo lako, Yahwe kwa sauti ya pumzi ya pua zako.
16 Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
Yeye alishuka chini kutokea juu; akanishikilia mimi! Akanivuta nje ya maji yafurikayo.
17 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
Aliniokoa kutoka kwa maadui zangu wenye nguvu, kutoka kwa wale ambao walinichukia mimi, kwa kuwa walikuwa na nguvu sana kuliko mimi.
18 Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini Bwana alikuwa msaada wangu.
Wao walikuja kinyume na mimi katika siku ile ya dhiki yangu lakini Mungu alikuwa msaada wangu!
19 Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
Yeye aliniweka huru katika eneo pana la wazi; yeye aliniokoa kwa sababu alipenezwa nami.
20 Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
Yahwe amenitunuku mimi kwa sababu ya haki yangu; yeye amenirejesha mimi kwa sababu mikono yangu ilikuwa misafi.
21 Kwa maana nimezishika njia za Bwana; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
Kwa kuwa nimezitunza njia za Yahwe na sijafanya uovu wa kumgeuka Mungu wangu.
22 Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake.
Kwa kuwa amri zake zote za haki zimekuwa mbele yangu; kama asemavyo, sijaenda kinyume nazo.
23 Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi.
Pia nimekuwa sina hatia mbele zake, na nimejiweka mwenyewe mbali na dhambi.
24 Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
Hivyo Yahwe amenirejesha kwa sababu ya haki yangu, na kwa sababu mikono yangu ilikuwa safi mbele ya macho yake.
25 Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia.
Kwa yeyote aliye mwaminifu, jionyeshe wenyewe kuwa mwaminifu; kwa mtu asiye na lawama, jionyeshe mwenyewe kuwa usiye na lawama.
26 Kwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi.
Kwa yeyote aliye msafi, jionyeshe mwenyewe safi; bali ni mjanja kwa yeyote aliye geuzwa.
27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini huwashusha wenye kiburi.
Kwa kuwa wewe huwaokoa watu walio taabishwa, lakini wewe huwashusha chini wale wenye majivuno, yaani macho yaliyo jinua!
28 Wewe, Ee Bwana, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka; Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
Kwa kuwa wewe huipa mwanga taa yangu; Yahwe Mungu wangu hutia mwanga giza langu.
29 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta.
Kwa kuwa kwa kupitia wewe ninaweza kuruka juu ya kiwazo kilichowekwa; kupitia Mungu ninaweza kuruka juu ya ukuta.
30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la Bwana halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.
Kama kwa Mungu: njia yake ni kamilifu. Neno la Yahwe ni safi! Yeye ni ngao kwa yeyote anaye kimbilia katika yeye.
31 Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya Bwana? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu?
Kwa kuwa nani ni Mungu ispokuwa Yahwe? Nani ndiye mwamba ispokuwa Mungu wetu?
32 Mungu ndiye anivikaye nguvu na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
Ni Mungu anitiaye nguvu ndani yangu kama vile mkanda, ambaye humweka mtu mwenye lawama katika njia yake.
33 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
Yeye hunifanya miguu yangu kuwa myepesi kama mbawala na kuniweka mahali pa juu!
34 Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
Yeye hufunza viganja vyangu kwa ajili ya vita na mikono yangu kupiga upinde wa shaba.
35 Hunipa ngao yako ya ushindi, nao mkono wako wa kuume hunitegemeza, unajishusha chini ili kuniinua.
Wewe umenipa mimi ngao ya wokovu. Mkono wako wa kuume umenisaidia, na neema yako imenifanya kuwa mkubwa.
36 Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze.
Wewe umetengeneza nafasi pana kwa ajili ya miguu yangu ili miguu yangu isiteleze.
37 Niliwafuatia adui zangu na nikawapata, sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
Ninawashawishi adui zangu na kuwakamata; nami sikurudi nyuma mpaka walipo haribiwa.
38 Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu.
Niliwashambulia hata hawakuweza kuamka; nao wameangukia chini ya miguu yangu.
39 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
Kwa kuwa unanitia nguvu kama mshipi kwa ajili ya vita; wewe unawaweka chini yangu wale ambao wanainuka kinyume na mimi.
40 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu.
Wewe ulinipa visogo vya maadui zangu; niliwaagamiza wale walio nichukia.
41 Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.
Wao waliita msaada lakini hakuna aliye wasaidia; walimuita Yahwe, lakini hakuwaitikia.
42 Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo; niliwamwaga nje kama tope barabarani.
Niliwapiga wao katika vipande vidogo vidogo kama vile vumbi mbele ya upepo; niliwatupa nje kama udongo mtaani.
43 Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa, watu ambao sikuwajua wananitumikia.
Wewe uliniokoa mimi kutoka katika migogoro ya watu. wewe umenifanya kichwa juu ya mataifa. Watu ambao sikuwahi kuwafahamu huntumikia.
44 Mara wanisikiapo hunitii, wageni hunyenyekea mbele yangu.
Pindi tu waliposikia kuhusu mimi, wao walinitii; wageni walilazimishwa kunisujudu.
45 Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
Wageni walitoka kwenye ngome yao wakitetemeka.
46 Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
Yahwe anaishi; mwamba wangu usifiwe. Ainuliwe Mungu wa wokovu wangu.
47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, awatiishaye mataifa chini yangu,
Yeye ni Mungu ambaye hutelekeza visasi kwa ajili yangu, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
48 aniokoaye na adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
Nimewekwa huru kutoka kwa adui zangu! wewe uliniinua juu ya wale walioinuka kunyume na mimi! Wewe uliniokoa kutoka kwa watu wenye vurugu.
49 Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee Bwana; nitaliimbia sifa jina lako.
Kwa hiyo nitakushukuru wewe, Yahwe, kati ya mataifa; Nitaliimbia sifa jina lako!
50 Humpa mfalme wake ushindi mkuu, huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.
Mungu hutoa ushindi mkuu kwa mfalme wake, na yeye huonyesha uaminifu wa agano lake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na ukoo wake milele.

< Zaburi 18 >