< Zaburi 15 >

1 Zaburi ya Daudi. Bwana, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu? 2 Ni yule aendaye pasipo mawaa, atendaye yaliyo haki, asemaye kweli toka moyoni mwake, 3 na hana masingizio ulimini mwake, asiyemtenda jirani yake vibaya, na asiyemsingizia mwenzake, 4 ambaye humdharau mtu mbaya, lakini huwaheshimu wale wamwogopao Bwana, yule atunzaye kiapo chake hata kama anaumia. 5 Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. Mtu afanyaye haya kamwe hatatikisika.

< Zaburi 15 >