< Zaburi 149 >

1 Msifuni Bwana. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watakatifu. 2 Israeli na washangilie katika Muumba wao, watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao. 3 Na walisifu jina lake kwa kucheza na wampigie muziki kwa matari na kinubi. 4 Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake, anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu. 5 Watakatifu washangilie katika heshima hii, na waimbe kwa shangwe vitandani mwao. 6 Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao na upanga ukatao kuwili mikononi mwao, 7 ili walipize mataifa kisasi na adhabu juu ya mataifa, 8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo, wakuu wao kwa pingu za chuma, 9 ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao. Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote. Msifuni Bwana.

< Zaburi 149 >