< Zaburi 137 >

1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza tulipokumbuka Sayuni. 2 Kwenye miti ya huko tulitundika vinubi vyetu, 3 kwa maana huko hao waliotuteka walitaka tuwaimbie nyimbo, watesi wetu walidai nyimbo za furaha; walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!” 4 Tutaimbaje nyimbo za Bwana, tukiwa nchi ya kigeni? 5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake. 6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu kama sitakukumbuka wewe, kama nisipokufikiri Yerusalemu kuwa furaha yangu kubwa. 7 Kumbuka, Ee Bwana, walichokifanya Waedomu, siku ile Yerusalemu ilipoanguka. Walisema, “Bomoa, Bomoa mpaka kwenye misingi yake!” 8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa, heri yeye atakayekulipiza wewe kwa yale uliyotutenda sisi: 9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga na kuwaponda juu ya miamba.

< Zaburi 137 >