< Zaburi 12 >

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Bwana tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu. 2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu. 3 Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno, 4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?” 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge na kulia kwa uchungu kwa wahitaji, nitainuka sasa,” asema Bwana. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.” 6 Maneno ya Bwana ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba. 7 Ee Bwana, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele. 8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati ambapo yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.

< Zaburi 12 >