< Zaburi 119 >

1 Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika sheria ya Bwana. 2 Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wao wote. 3 Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake. 4 Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu. 5 Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako! 6 Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote. 7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki. 8 Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa. 9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako. 10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako. 11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi. 12 Sifa ni zako, Ee Bwana, nifundishe maagizo yako. 13 Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako. 14 Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi. 15 Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako. 16 Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako. 17 Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako. 18 Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. 19 Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako. 20 Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa juu ya sheria zako wakati wote. 21 Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa waendao mbali na amri zako. 22 Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako. 23 Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. 24 Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu. 25 Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 26 Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako. 27 Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako. 28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako. 29 Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako. 30 Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako. 31 Nimengʼangʼania sheria zako, Ee Bwana, usiniache niaibishwe. 32 Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru. 33 Ee Bwana, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika mpaka mwisho. 34 Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote. 35 Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha. 36 Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. 37 Geuza macho yangu kutoka kwenye mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 38 Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa. 39 Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema. 40 Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako. 41 Ee Bwana, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako, 42 ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako. 43 Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako. 44 Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele. 45 Nitatembea nikiwa huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. 46 Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa, 47 kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda. 48 Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako. 49 Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini. 50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu. 51 Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako. 52 Ee Bwana, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji. 53 Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako. 54 Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi. 55 Ee Bwana, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako. 56 Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako. 57 Ee Bwana, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako. 58 Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako. 59 Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako. 60 Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako. 61 Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako. 62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki. 63 Mimi ni rafiki kwa wale wote wakuchao, kwa wote wanaofuata mausia yako. 64 Ee Bwana, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako. 65 Mtendee wema mtumishi wako Ee Bwana, sawasawa na neno lako. 66 Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako. 67 Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako. 68 Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako. 69 Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote. 70 Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako. 71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako. 72 Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu. 73 Mikono yako ilinifanya na kuniumba, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako. 74 Wakuchao wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako. 75 Ee Bwana, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu. 76 Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. 77 Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako. 78 Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako. 79 Wale wakuchao na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako. 80 Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe. 81 Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako. 82 Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifajiri lini?” 83 Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako. 84 Mtumishi wako itampasa angoje mpaka lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu? 85 Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako. 86 Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu. 87 Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako. 88 Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako. 89 Ee Bwana, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni. 90 Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu. 91 Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia. 92 Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu. 93 Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu. 94 Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako. 95 Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako. 96 Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mpaka. 97 Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu. Ninaitafakari mchana kutwa. 98 Amri zako zimenipa hekima zaidi kuliko adui zangu, kwa kuwa nimezishika daima. 99 Nina akili zaidi kuliko walimu wangu wote, kwa kuwa ninatafakari juu ya sheria zako. 100 Nina ufahamu zaidi kuliko wazee, kwa kuwa ninayatii mausia yako. 101 Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya, ili niweze kutii neno lako. 102 Sijaziacha sheria zako, kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe. 103 Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu! 104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako, kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu. 105 Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu. 106 Nimeapa na nimethibitisha, kwamba nitafuata sheria zako za haki. 107 Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Bwana, sawasawa na neno lako. 108 Ee Bwana, pokea sifa za hiari za kinywa changu, nifundishe sheria zako. 109 Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote, sitasahau sheria yako. 110 Waovu wamenitegea mtego, lakini sijayakiuka maagizo yako. 111 Sheria zako ni urithi wangu milele, naam ni furaha ya moyo wangu. 112 Nimekusudia moyoni mwangu kuyafuata maagizo yako mpaka mwisho. 113 Ninachukia watu wa nia mbili, lakini ninapenda sheria yako. 114 Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu, nimeweka tumaini langu katika neno lako. 115 Ondokeni kwangu, ninyi mtendao mabaya, ili niweze kushika amri za Mungu wangu! 116 Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi; usiache matumaini yangu yakavunjwa. 117 Nitegemeze, nami nitaokolewa, nami daima nitayaheshimu maagizo yako. 118 Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure. 119 Waovu wa nchi unawatupa kama takataka, kwa hivyo nazipenda sheria zako. 120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe, ninaziogopa sheria zako. 121 Nimetenda yaliyo haki na sawa, usiniache mikononi mwa watesi wangu. 122 Mhakikishie mtumishi wako usalama, usiache wenye kiburi wanionee. 123 Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako, na kuitazamia ahadi yako ya kweli. 124 Mfanyie mtumishi wako kulingana na upendo wako na unifundishe maagizo yako. 125 Mimi ni mtumishi wako; nipe ufahamu ili niweze kuelewa sheria zako. 126 Ee Bwana, wakati wako wa kutenda umewadia, kwa kuwa sheria yako inavunjwa. 127 Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi, 128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili, nachukia kila njia potovu. 129 Sheria zako ni za ajabu, hivyo ninazitii. 130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru, kunampa mjinga ufahamu. 131 Nimefungua kinywa changu na kuhema, nikitamani amri zako. 132 Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote wale wanaolipenda jina lako. 133 Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako, usiache dhambi yoyote initawale. 134 Niokoe na uonevu wa wanadamu, ili niweze kutii mausia yako. 135 Mwangazie mtumishi wako uso wako na unifundishe amri zako. 136 Chemchemi za machozi zinatiririka kutoka machoni yangu, kwa kuwa sheria yako haifuatwi. 137 Ee Bwana, wewe ni mwenye haki, sheria zako ni sahihi. 138 Sheria ulizoziweka ni za haki, ni za kuaminika kikamilifu. 139 Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu wanayapuuza maneno yako. 140 Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu, mtumishi wako anazipenda. 141 Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa, sisahau mausia yako. 142 Haki yako ni ya milele, na sheria yako ni kweli. 143 Shida na dhiki zimenipata, lakini amri zako ni furaha yangu. 144 Sheria zako ni sahihi milele, hunipa ufahamu ili nipate kuishi. 145 Ee Bwana, ninakuita kwa moyo wangu wote, nami nitayatii maagizo yako. 146 Ninakuita; niokoe nami nitazishika sheria zako. 147 Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada; nimeweka tumaini langu katika neno lako. 148 Sikufumba macho yangu usiku kucha, ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako. 149 Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako, Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na sheria zako. 150 Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami, lakini wako mbali na sheria yako. 151 Ee Bwana, hata hivyo wewe u karibu, na amri zako zote ni za kweli. 152 Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako kwamba umezithibitisha ili zidumu milele. 153 Yaangalie mateso yangu, uniokoe, kwa kuwa sijasahau sheria yako. 154 Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako. 155 Wokovu uko mbali na waovu, kwa kuwa hawatafuti maagizo yako. 156 Ee Bwana, huruma zako ni kuu, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako. 157 Adui wanaonitesa ni wengi, lakini mimi sitaziacha sheria zako. 158 Ninawatazama wasioamini kwa chuki, kwa kuwa hawalitii neno lako. 159 Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako; Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na upendo wako. 160 Maneno yako yote ni kweli, sheria zako zote za haki ni za milele. 161 Watawala wamenitesa bila sababu, lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako. 162 Nafurahia ahadi zako kama mtu aliyepata mateka mengi. 163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako. 164 Ninakusifu mara saba kwa siku, kwa ajili ya sheria zako za haki. 165 Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza. 166 Ee Bwana, ninangojea wokovu wako, nami ninafuata amri zako, 167 Ninazitii sheria zako, kwa sababu ninazipenda mno. 168 Nimetii mausia yako na sheria zako, kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako. 169 Ee Bwana, kilio changu na kifike mbele zako, nipe ufahamu sawasawa na neno lako. 170 Maombi yangu na yafike mbele zako, niokoe sawasawa na ahadi yako. 171 Midomo yangu na ibubujike sifa, kwa kuwa unanifundisha maagizo yako. 172 Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, kwa kuwa amri zako zote ni za haki. 173 Mkono wako uwe tayari kunisaidia, kwa kuwa nimechagua mausia yako. 174 Ee Bwana, ninatamani wokovu wako, na sheria yako ni furaha yangu. 175 Nijalie kuishi ili nipate kukusifu, na sheria zako zinitegemeze. 176 Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea. Mtafute mtumishi wako, kwa kuwa sijasahau amri zako.

< Zaburi 119 >